Morogoro yatafuta dawa ya mashabiki wakorofi viwanjani

Muktasari:

Mashabiki wamekuwa na tabia ya kutoa lugha za maudhi, kejeli na matusi ya nguoni kwa waamuzi wanaochezesha michezo mbalimbali ya kusaka bingwa wa mkoa wa Morogoro.

Morogoro.Chama cha soka mkoa wa Morogoro (MRFA) kimechukizwa na tabia za baadhi ya mashabiki wanaowakejeli na kuwatusi waamuzi wanaochezesha ligi daraja la tatu mkoa Morogoro kwenye Uwanja wa Sabasaba.

Mashabiki wamekuwa na tabia ya kutoa lugha za maudhi, kejeli na matusi ya nguoni kwa waamuzi wanaochezesha michezo mbalimbali ya kusaka bingwa wa mkoa wa Morogoro 2019/2020.

Katibu msaidizi wa MRFA, Jimmy Lengwe alisema tayati jopo inayosimamia michezo ya ligi hiyo imeanza kuwachukulia hatua baadhi ya mashabiki wanatoa lugha za kashfa na matusi ya nguoni kwa waamuzi.

Lengwe alisema kuwa baadhi ya mashabiki wa timu ya Burkina Fc wamechukuliwa hatua ya kuonywa na chama hicho lengo kuufanya mchezo wa soka uendelea kutoa burudani kwa rika zote.

“Uwanja wa Sabasaba umekuwa ukiingiza mashabiki wa kila aina wakiwemo wanawake, wanaume na watoto, lakini imezuka tabia ya baadhi ya watu kutoa lugha za kashfa na matusi ya nguoni kwa waamuzi na jambo hili hatuwezi kulivumilia tutachukua hatua kukomesha hii tabia.’alisema Lengwe.

Lengwe amemtaja shabiki wa Dakawa Rangers ya Mvomero, Mpolokile Paul kuwa ni mmoja wa mashabiki wenye kutoa lugha za kashfa na matusi ya nguoni na tayari ameonywa na chama.

“Mwandishi wewe ni shahidi umeona namna tunavyopambana na shabiki wanaotoa lugha zisizo za kiungwana dhidi ya waamuzi na huyu, Mpolokile Paul tumekuwa tukimfuatilia kuanzia mchezo dhidi ya Mkundi United na mchezo huu wa leo (jana) na hawa Kihonda United amekuwa akitoa lugha kali za matusi ya nguoni na kashfa kwa waamuzi,”alisema Lengwe.

Lengwe alisema tayari ameonywa na endapo akionyesha tabia hiyo, chama hakitasita kumchukulia hatua ikiwemo kumfungulia mashtaka.

Akizungumzia suala hilo la shabiki huyo wa Dakawa Rangers, Mpolokile Paul alisema kuwa mashabiki wa mjini wamekuwa wakimchokoza kwa kumtusi na anachofanya yeye ni kujibu mashambulizi.

“Nimekuwa nikitukanwa mimi na mashabiki wa timu za mjini baada ya kuwakosoa waamuzi kwani wamekuwa wakipindisha sheria 17 za mchezo wa soka na timu yetu ya Dakawa Rangers kunyimwa haki katika maamuzi ndio sababu ya mimi kuonywa,’alisema Mpolokile.

Katika michezo ya Dakawa Rangers tayari imepoteza miwili mbele ya Mkundi United ikichapwa mabao 2-1 kabla ya mchezo wa jana (juzi) kupoteza tena kwa kutandikwa mabao 2-0.