Morata adai wachezaji Chelsea wamemvuruga

Muktasari:

Fowadi huyo alisajiliwa na Chelsea kwa ada ya Pauni 65 milioni mwaka 2017. Mambo hayakuwa mazuri kwake na kumfanya aishie kuanzishwa mara 35 tu kwenye mechi za Ligi Kuu England na kutimkia Atletico katikati ya msimu uliopita.

MADRID, HISPANIA . STRAIKA Alvaro Morata amesema wachezaji wenzake wa Chelsea walimtia wazimu kwa sababu walimfanya ahisi hajui mpira.

Straika huyo wa Kihispaniola akiwa kwa mkopo Atletico Madrid, huku kukiwa na uwezekano wa kubebwa jumla kwa Pauni 58 milioni mwakani, maisha yake Stamford Bridge yalikuwa ovyo huku wachezaji wenzake wa The Blues wakimfanya ajione hakuwa na uwezo wa kuufanyia mpira jambo lolote zuri ndani ya uwanja.

Morata, 27, aliambia COPE Radio ya Hispania: “Nina furaha kwa sasa. Hakikuwa kipindi kizuri katika maisha yangu ya soka, sikuwa nafurahia kabisa. Ilifika kipindi hata mimi mwenyewe nilikuwa sijiamini.”

Fowadi huyo alisajiliwa na Chelsea kwa ada ya Pauni 65 milioni mwaka 2017. Mambo hayakuwa mazuri kwake na kumfanya aishie kuanzishwa mara 35 tu kwenye mechi za Ligi Kuu England na kutimkia Atletico katikati ya msimu uliopita.

Alifunga mabao 15 kwa miezi 18 aliyocheza kwenye Ligi Kuu England na hivyo kushindwa kumshawishi Kocha Maurizio Sarri au aliyekuwa mtangulizi wake Antonio Conte.

Kufuatia Chelsea kufungiwa kusajili, wengi walidhani Kocha Frank Lampard angezuia uhamisho huo wa Atletico, lakini aliruhusu na kuamua kubaki na mastraika wengine Tammy Abraham, Michy Batshuayi na Olivier Giroud.

Kwa sasa Morata amekuwa moto kwelikweli huko Atletico akifunga katika mechi 13 alizochezea kikosi hicho cha Kocha Diego Simeone, huku akifunga kwenye mechi sita mfululizo.