Monaco yamnasa muuaji wa Sevilla, Ben Yedder

Muktasari:

Ben Yedder katika miaka mitatu aliyocheza Sevilla amefunga mabao 70 katika mechi 138, za mashindano yote.

Paris, Ufaransa. Mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa, Wissam Ben Yedder amejiunga na Monaco akitokea Sevilla kwa mkataba wa miaka mitano.

Ben Yedder alikuwa akihusishwa na kutakiwa na Manchester United kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili Agosti 8, lakini ameweza kuhama kutoka Hispania kwenda Ufaransa ambao bado hawajafunga usajili wao.

Monaco ilimaliza vibaya msimu uliopita wa Ligue 1, ikishika nafasi ya 17, ikiwa juu kwa pointi mbili kutoka katika janga la kushuka daraja, baada ya msimu 2017-18 kumaliza nafasi nafasi ya pili nyuma ya mabingwa PSG.

Katika dirisha hili Monaco wamekuwa katika jitihada kubwa za kujenga kikosi chake kwa kumsajili Henry Onyekuru kutoka kwa Everton na kuwakopesha Djibril Sidibe, huku wakimuuza Youi Tielemans kwa Leicester.

Ben Yedder ni mchezaji mpya aliyewasili baada ya kucheza kwa miaka mitatu Sevilla, akiwa amefunga mabao 70 katika mechi 138, za mashindano yote.

 

Mshambuliaji huyo mwenye miaka 29, amewahi kucheza Ufaransa kwa miaka sita katika klabu ya Toulouse akiwa amefunga mabao 63, katika mechi 156 za Ligue 1.

"Nimefurahi kuhushwa na AS Monaco," Ben Yedder aliambia tovuti ya klabu hiyo. "Najiona mwenye bahati kwa kufuatwa na klabu hii.

"Nimeichagua Monaco kwa sababu naamini ina mipango mikubwa na naamini nitafanya kila niwezalo kutimiza malengo yetu.

"Nimekuja kwa lengo la kuthibisha ubora wangu, wakati wote matamanio yangu ni kufikia malengo ya juu zaidi.

"Napenda kushuruku kwa klabu kwa kuniamini. Ni siku nzuri inayoanza na hadithi mpya ndicho kitu nisichotaka kupoteza muda kuanza."