Monaco ya Thierry Henry yachezea vichapo hadi aibu

Muktasari:

  • Kocha mpya wa Monaco, Thierry Henry amesema licha ya kuwa na mwanzo mbaya lakini anamatumaini ya kufanya vizuri katika mechi zijazo, akiwa hajashinda mchezo hata mmoja tangu atwae mikoba hiyo Oktoba 18, ameambulia sare mbili na kupoteza mechi nne.

Monaco, Ufaransa. Mambo yamemwendea vibaya kocha mpya wa Monaco, Thierry Henry, baada ya jana kushuhudia timu yake ikipoteza mchezo wa nne kati ya sita aliyoiongoza ilipofungwa mabao 4-0 na PSG katika mechi ya Ligi Kuu Ufaransa.

Henry aliteuliwa kwa matumaini makubwa na bilionea anayeimiliki timu hiyo Dmitry Rybolovlev, kuchukua nafasi iliyoachwa na Leonardo Jardim, ambaye aliipa timu hiyo ubingwa msimu wa 2016/17 na msimu uliopita ilikuwa ya pili lakini aliuanza msimu huu vibaya.

Hata hivyo mbinu za Henry zinaonekana kufeli baada ya mshambuliaji mahiri wa Uruguay, Edinson Cavani kufunga mabao matatu ‘hat-trick’ na Neymar akifunga kwa penalti kuiwezesha PSG kushinda mechi zote 13 ilizocheza za Ligue 1 msimu huu.

Pengine ilikuwa bahati kubwa kwa Henry baada ya teknolojia ya kusaidia kuondoa utata wa mabao (VAR) kuyakataa mabao ya Julian Draxler na Kylian Mbappe vinginevyo angefungwa 6-0.

Kipigo hicho ni cha pili kwa Monaco kufungwa mabao 4-0 ikiwa nyumbani ndani ya wiki moja kwani ilifungwa mabao kama hayo na Club Brugge ya Ubelgiji katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya katikati ya wiki iliyopita.

Henry ambaye alipata kuitumikia Monaco enzi zake za uchezaji wake kabla ya kuhamia Juventus na baadaye Arsenal alikopata jina, alitangazwa kuwa kocha Oktoba 18 mwaka huu, ambapo alipoteza mchezo wake wa kwanza uliochezwa siku mbili baadaye alipofungwa 2–1 na Strasbourg.

Chini yake timu hiyo imeambulia sare katika mechi moja na kupoteza mitatu ya Ligi Kuu Ufaransa na huku ikipoteza mchezo mmoja na kutoka sare mmoja katika Ligi ya Mabingwa Ulaya yote dhidi ya Club Brugge.

Monaco, iliyomaliza msimu uliopita ikiwa nafasi ya pili, msimu huu inapigania kutoshuka daraja ikishika nafasi ya pili kutoka mkiani baada ya kushinda mchezo mmoja, kutoka sare minne na kupoteza michezo minane.

Vijana wa Henry, wameachwa kwa pointi 31 na vinara wa ligi hiyo PSG zikiwa zimebakia mechi sita kabla ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza, lakini kocha huyo amesema anaamini timu hiyo itazinduka na kushinda mechi zijazo.

'Kuna kitu kinachangia sisi kufanya vibaya nalo ni kuandamwa na majeruhi, mfano katika mchezo huu ‘jana’ Nacer Chadli aliumia tukalazimika kumtoa, Radamel Falcao naye hayupo fiti tunapitia kipindi kigumu kidogo,” alisema Henry.

Kocha huyo alisema anapata matumaini kidogo baada ya kuona timu inatengeneza nafasi za kufunga akasema Jordi Mboula, aliyeingia badala ya Chadli angeweza kuifungia bao lakini akashindwa kufanya hivyo licha ya kuingia ndani ya 18 na kipa wa PSG kutoka langoni.

“Ukiangalia namna tulivyocheza dhidi ya PSG utabaini kuwa tunaweza kufanya vizuri katika michezo ijayo, kwa sababu licha ya kucheza na timu bora lakini tulitengeneza nafasi kadhaa ingawa hatukuzitumia,” alisema.