Monaco imepiga bei mastaa wa maana chini ya Kocha Jardim

Muktasari:

Kocha Leonardo Jardim ameiruhusu AS Monaco kuwapiga bei mastaa 10 ambao wangeifanya timu hiyo kuwa tishio zaidi Ulaya na badala yake wameenda kuzinufaisha klabu nyingi

MONACO kwa sasa imemfuta kazi Kocha Leonardo Jardim na kumpa majukumu hayo staa wa zamani wa timu hiyo na Arsenal, Thierry Henry.
Wakati Jardim akiwa kwenye kikosi cha Monaco amepata kuwa na kikosi kilichokuwa na mastaa kibao wa maana ambao waliitikisa Ulaya, lakini kitu cha kushangaza alikubali kuwapiga bei kwenda kuzinufaisha timu nyingine za Ulaya.
Hii ndio orodha ya masupastaa wa maana ambao Kocha Jardim amewapiga bei akiwa kwenye kikosi hicho cha Monaco na kuwafanya kushuka ubora wao unaowafanya wateswe na wapinzani wao huko kwenye Ligue 1 na Ligi ya Mabingwa Ulaya.  Hata hivyo, Monaco imepiga pesa kibao kwa kuuza mastaa hao.

10.Yannick Carrasco
Atletico Madrid
Ada: Pauni 22.5 milioni
Carrasco alisajiliwa na Monaco akiwa na umri wa miaka 17 tu akitokea Genk mwaka 2010. Baada ya kutua kwenye kikosi hicho cha Monaco, Carrasco alionyesha kiwango kikubwa sana na kuwa sehemu muhimu ya timu hiyo hasa baada ya Kocha Jardim kutua kwenye timu hiyo.
Lakini cha ajabu Jardim alimuuza mchezaji huyo kwenda Atletico Madrid alikofanya mambo makubwa kabla ya Wahispaniola hao kumuuza kwenda Dalian Yifang ya China.

9. Geoffrey Kondogbia
Inter Milan
Ada: Pauni 27 milioni
Kondogbia alijiunga na Monaco wakati inapanda daraja mwaka Monaco akitokea huko Hispania, ambako alikuwa akiitumikia Sevilla. Kipindi hicho, Monaco ilikuwa chini ya Kocha Claudio Ranieri na Kondogbia alikwenda kuikamatia kiungo ya timu hiyo. Kisha Monaco ikamchukua Kocha Jardim na alipata nafasi ya kufanya kazi na Kondogbia kabla ya kumuuza kwenda Inter Milan. Kwa sasa Kondogbia amerudi Hispania akikipiga Valencia.

8.Tiemoue Bakayoko
Chelsea
Ada: Pauni 40 milioni
Mmoja kati ya mastaa matata kwenye kikosi cha Monaco kilichobeba ubingwa wa Ufaransa mwaka 2017. Bakayoko aling'ara kwelikweli huko Stade Louis II kabla ya kukutana na majeraha ambayo yalitibua maisha yake baada ya kuuzwa huko Chelsea.
Lakini jambo kubwa hapa ni kitendo cha Kocha Jardim kukubali kumuuza staa huyo muhimu. Kwa sasa Bakayoko yupo kwa mkopo AC Milan akitokea Chelsea licha ya mambo yake si mazuri huko.

7.Fabinho
Liverpool
Ada: Pauni 40.5 milioni
Kiraka huyo wa Kibrazili alikuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Kocha Jardim huko Monaco hasa ilipobeba ubingwa wa Ligue 1 mwaka 2017.
Monaco ilimnasa Fabinho kwa mkopo kutoka Rio Ave kabla ya kumbeba jumla na kuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi hicho ambapo wakati mwingine alikuwa akitumika kama kiungo mkabaji na muda mwingine beki wa kulia. Fabinho alikuwa askari mwaminifu kwa Jardim sasa yupo Liverpool.

6.Bernardo Silva
Man City
Ada: Pauni 45 milioni
Staa huyo wa Ureno, Bernardo Silva kwa sasa anafanya mambo yake kwenye kikosi cha Manchester City, lakini aliwahi kupita kwenye kikosi cha Monaco. Awali alijiunga na timu hiyo kwa mkopo, lakini baada ya miezi sita tu, Monaco ikaamua kumbeba jumla kutokana na kunogewa na huduma yake. Silva akawa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Jardim, lakini pia akashindwa kumzuia asiondoke na Man City ikamnasa.

5.Benjamin Mendy
Man City
Ada: Pauni 51.75 milioni
Mendy alikuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Jardim, lakini naye ni mmoja kati ya wachezaji waliopigwa bei na timu hiyo ya Monaco na sasa anafanya mambo yake kwenye timu nyingine.
Hakuna ubishi, Jardim alikuwa na kikosi kilichokuwa kimesheheni mastaa wakali watupu huko Monaco, lakini mmoja baada ya mwingine aliruhusu waondoke, wakiuzwa kwa pesa nyingi kwenda kuimarisha klabu nyingine za Ulaya.

4.Anthony Martial
Man United
Ada: Pauni 54 milioni
Akitajwa kuwa Thierry Henry mpya, Martial alikuwa kwenye kiwango kizuri sana wakati anaibukia huko Napoli iliyokuwa chini ya Jardim, ambapo alicheza mechi 48 na kufunga mabao 12 katika michuano tofauti kwenye msimu wa 2014/15.
Lakini Jardim hakutaka kufanya kazi ya ziada kumzuia staa wake huyo asiondoke wakati Manchester United ilipoenda kutaka huduma yake, ikamsajili.

3.Thomas Lemar
Atletico Madrid
Ada: Pauni 63 milioni
Alihusishwa na timu kibao kwenye dirisha lililopita kabla ya kiungo huyo wa Ufaransa kuamua kwenda kujiunga na Atletico Madrid ya Hispania.
Lemar ni staa mwingine mwenye kipaji cha juu ambaye alipigwa bei na Monaco chini ya Kocha Jardim.
Alikuwa silaha muhimu kwenye kikosi hicho cha Ufaransa na huko alikokwenda msimu huu amecheza mechi 10, akifunga mara mbili na kuasisti mara mbili, si haba.

2.James Rodriguez
Real Madrid
Ada: Pauni 67.5 milioni
James alikuwa kwenye kiwango bora sana wakati anaondoka Monaco kwenda Real Madrid baada ya fainali za Kombe la Dunia 2014 zilizofanyika Brazil. Hata hivyo, staa huyo wa Colombia aliondoka kwenye kikosi hicho cha Monaco akiwa hajacheza mechi yoyote chini ya Kocha Jardim.
Kwa sasa yupo kwa mkopo huko Bayern Munich, ambako amedaiwa kuwa katika uhusiano mbaya na Kocha Nico Kovac.

1.Kylian Mbappe
Paris Saint-Germain
Ada: Pauni 166 milioni
Jiwe la dhahabu hili lililokuwapo kwenye kikosi cha AS Monaco. Hakika, Kylian Mbappe ni mchezaji wa kiwango cha juu sana ambaye Monaco ilimuuza na kitu kibaya imemuuza kwa wapinzani wao wa ndani ya Ligi Kuu Ufaransa, Paris Saint-Germain.
Akiwa na Monaco, Mbappe alifunga mabao 26 na kuasisti mara nane katika michuano yote na hicho kiliifanya PSG juu kutoa pesa ndefu kumsajili.