Mohamed Kassim Afichua siri ya kuwakaba Kagere, Morrison

Muktasari:

Mwanaspoti lilifanya mahojiano na beki huyo ambapo alieleza namna anavyojipanga kabla ya mechi ikiwemo mazoezi ya kujiweka fiti huku akifichua mambo kadha wa kadha.

KAMA unatunza kumbukumbu kwenye mechi ya Simba na Polisi Tanzania iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na mabingwa watetezi walishinda mabao 2-1, ni lazima Mohamed Kassim utamkumbuka kwa kiwango alichoonyesha siku hiyo.

Kassim ni beki ambaye alimudu vyema mchezo huo na kuwadhibiti washambuliaji wa Simba, Meddie Kagere na John Bocco ambao walionekana kuwa wasumbufu kwa Polisi.

Ukiachana na mechi hiyo, Kassim pia alionyesha kiwango bora alipokutana na safu ya ushambuliaji ya Azam kwa kumdhibiri straika wao, Obrey Chirwa huku akimbana mshambuliaji wa Yanga, Bernard Morrison walipokutana katika mechi zao za Ligi Kuu Bara.

Mwanaspoti lilifanya mahojiano na beki huyo ambapo alieleza namna anavyojipanga kabla ya mechi ikiwemo mazoezi ya kujiweka fiti huku akifichua mambo kadha wa kadha.

Majeruhi yamkwamisha

Safari ya mchezaji huyo kuingia Ligi Kuu haikuwa nyepesi kwani wachezaji ni wengi na wenye uwezo.

Kassim anasema alianza kujikomaza kupitia Coastal Union ilipokuwa inashiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL), na alifanikiwa kuipandisha.

“Nilicheza Coastal na ikapanda Ligi Kuu, lakini nilipata majeraha mechi ya mwisho, hivyo timu ilivyopanda nilijikuta nipo mtaani tu lakini usajili wa dirisha dogo ndio nilienda kuipambania Polisi Tanzania mpaka tukapanda msimu huu,” anasema.

“Majeruhi ni kama yalinichelewesha kucheza ligi lakini naichukulia kama changamoto na huwezi kujuwa Mungu alipanga nini.”

Matizi yake

Kassim anasema akiwa nyumbani ratiba yake ni kukimbia kwa siku tatu umbali mrefu na siku zinazobaki huzitumia kucheza mpira.

“Mazoezi nafanya mara moja tu kwa siku ninapokuwa nyumbani, lakini nikiwa kambini huwa naangalia ratiba ya mwalimu ikiwa hainibani najiongeza sana kufanya mazoezi yangu binafsi kwa sababu nataka kuwa fiti muda wote,” anasema na kuongeza kwamba, ratiba ikimruhusu huwa anafanya mazoezi ya gym kwani eneo analocheza uwanjani anatumia nguvu zaidi.

Nyoni na Ramos

Kassim, bila kupepesa macho anamtaja kiraka wa Simba, Erasto Nyoni ndiye mchezaji anayemkubali ndani ya Ligi Kuu Bara kwa namna ambavyo anacheza.

“Nyoni anapokuwa uwanjani kila mmoja anapenda vile anavyocheza, ni mtu mwenye umakini sana kwenye kukaba, lakini ni mtulivu, ndio maana hata mimi nakuwa mtulivu kwa sababu najifunza vitu kupitia yeye,” anasema.

Beki huyu anaongeza kuwa upande kwa mchezaji wa nje anavutiwa zaidi na beki wa Real Madrid, Sergio Ramos.

“Ramos ni beki ambaye anatumia sana akili anapokuwa uwanjani hasa kwenye kukaba, pia anacheza kwa kujitolea ndani ya timu.”

Anawaza nje

Kama ilivyo kwa wachezaji wengi kuhitaji kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, basi ndivyo ilivyo kwa beki huyu.

Kassim anafichua hataki kucheza muda mrefu bali anataka kupata uzoefu kisha kwenda zake nje.

“Nina ndoto ya kucheza nje na umri wangu unaruhusu, nimezaliwa 1996 na hii ni mara yangu ya kwanza kucheza ligi, lakini tayari nina ndoto zangu, hivyo naamini kila kitu kitakuwa sawa,” anasema.

Kagere, Chirwa, Morrison

Katika mechi za Polisi Tanzania dhidi ya Yanga, Azam na Simba, Kassim alionyesha utulivu pamoja na beki mwenzake Idd Mobby kuhakikisha wanawakaba vilivyo washambuliaji hao.

Beki huyo anayevaa jezi namba tano mgongoni alitumia nguvu kuhakikisha washambuliaji hao hawatambi kwenye michezo baina yao walipokutana.

“Unajua mechi kama hizo mwalimu anakupa maelekezo ya namna unavyoweza kukabiliana na wachezaji wenye uwezo, tuliambiwa tusiwape nafasi kubwa na ndio maana uliona tuliwakaba vilivyo, baada ya kufanya kile ambacho tunaelekezwa hata kwenye mechi ya Yanga najua uliona Morrison hakuwa kama alivyocheza mechi zote.”

Aitaka Chan

Siku si nyingi Tanzania itakuwa na kibarua kigumu katika Fainali Zinazowahusisha Wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (Chan), wakati Kocha Ettiene Ndayiragije akiwa anazunguka kutafuta wachezaji, basi Kassim anatamani nafasi hiyo imwangukie.

“Unajua kila mchezaji anataka kucheza timu ya Taifa, hata upande wangu ipo hivyo, lakini unajua nafasi yetu wapo wengi wenye uwezo ngoja tuone itakavyokuwa,” anasema.

Mapumziko na familia

Wachezaji wa Ulaya wanapokuwa mapumziko huwa wanaonekana kwenye fukwe za Ibiza (Hispania) pamoja na Dubai wakila bata na warembo wao.

Kibongobongo hapa unakuta ni vigumu kwa mchezaji kufanya hivyo na hata beki huyo anakubaliana na ukweli huo kwa kutokuwa tofauti akisema muda wake wa mapumziko huutumia kutembelea ndugu.

“Mapumziko yangu huwa natumia kuwatembelea ndugu na marafiki zangu, napenda kukaa nao pamoja kisha kubadilishana mawazo,” anasema.