Mogella awataka mashabiki kujitokeza kwa wingi viwanjani

Muktasari:

Mashabiki wa soka nchini wameombwa kuziunga mkono timu zote nne zinazoshiriki michuano ya kimataifa.

Dar es Salaam. Nyota wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella amesema timu zinazoshiriki mashindano ya kimataifa zipo kwa ajili la kuliwakisha taifa, hivyo ni wajibu wa kila shabiki kuunga mkono.

Mogella alisema ni jambo la kujivunia kuona Simba, Yanga, Azam FC na KMC zinabeba uhalisia wa soka la Tanzania dhidi ya timu wanazocheza nazo, akidai itakuwa inawapa nafasi kubwa wachezaji kutanua ajira zao.

Alisema Simba na Yanga ndizo zenye mashabiki wa kutosha, jambo alilowaomba kuaunga mkono Azam FC na KMC kwamba uwepo wao utawafanya wachezaji kuwapa moyo wa kujituma kwa bidii.

"Ushabiki wa Simba na Yanga tuuweke pembeni, hii ni mara ya kwanza kucheza timu nne kimataifa, lazima tuamke kutoka usingizini kuzisapoti ili ziweze kufika mbali.

"Pamoja na matokeo ambayo wameyapata awali haina maana kwamba hawawezi kuyabadili kwenye mechi zao za marudiano, kikubwa wajengewe imani kwamba wanaweza na wataweza, wakifanya vyema wanaliletea taifa sifa," alisema Mogella.