Mogela atoa ya moyoni kipigo cha Taifa Stars

Muktasari:

  • Taifa Stars watacheza mchezo wa pili Juni 27, dhidi ya majirani zake Kenya ambao nao katika mchezo wa kwanza jana usiku walikubali kufungwa mabao 2-0, dhidi ya Algeria

Dar es Salaam.Timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' imecheza mchezo wake wa kwanza katika kombe la Mataifa Afrika dhidi ya Senegal 'Simba wa Telanga' na kukubali kufungwa mabao 2-0 katika Kundi C.

Baada ya kupoteza mchezo huo mshambuliaji wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Zamoyoni Mogela 'Golden Ball' alisema Stars ilipoteza mechi hiyo kutokana na uzoefu wa Senegal.

Mogela alisema Senegal wana wachezaji wengi mbali ya uzoefu waliokuwa nao kucheza mashindano hayo lakini wamekuwa katika misingi na makuzi ya kisoka ambayo kwao kucheza na timu kama Taifa Stars ilikuwa lazima watuzidi katika maeneo mengi na ndio ilivyokuwa.

"Makosa yalikuwepo haswa katika eneo la kiungo tulikuwa tukipoteza mipira mingi ambayo ilikuwa faida kwa wenzetu, lakini miongoni mwa eneo ambalo katika mchezo na Senegal tulikuwa bora ni katika safu ya ulinzi haswa ikiongozwa na kipa Aishi Manula ambaye kama si uimara wake kulikuwa na mabao mengi  yakufungwa," alisema.

"Sehemu nyingine ambayo hatukuwa vizuri ni katika safu ya ushambuliaji ilionekana kuzidiwa pengine kutokana kutokuwa wanapata mipira mengi kwa sababu viungo walikuwa wamezidiwa na wa timu pinzani.

"Bado tusikate tamaa kuna nafasi ambayo tunayo kama tutafanyia kazi makosa yetu hayo ya mchezo uliopita dhidi ya Kenya kwenye mechi inayofata ambao tumezoeana nao tunaweza kupata matokea ya ushindi na tukawa katika nafasi nzuri ya kuendelea mbele," alisema Mogela.

Taifa Stars watacheza mchezo wa pili Juni 27, dhidi ya majirani zake Kenya ambao nao katika mchezo wa kwanza jana usiku walikubali kufungwa mabao 2-0, dhidi ya Algeria.