Mogela ataka Serengeti wajipime Afrika Kaskazini

Muktasari:

  • Kauli hiyo imetolewa na mshambuliaji wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Zamoyoni Mogela na timu za nchi hizo ni nzuri kujipima nazo kwa madai zimeshiriki mashindano mengi na viwango vyao vipo juu hivyo zitawapa uzoefu Serengeti Boys.

KUELEKEA michuano ya Kombe la Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 (AFCON) inayotarajiwa kuanza mwezi ujao nchini, imeelezwa kikosi cha timu ya Taifa ya vijana Serengeti Boys kijipime na timu za Afrika Kaskazini na Magharibi.

Kauli hiyo imetolewa na mshambuliaji wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Zamoyoni Mogela na timu za nchi hizo ni nzuri kujipima nazo kwa madai zimeshiriki mashindano mengi na viwango vyao vipo juu hivyo zitawapa uzoefu Serengeti Boys.

Alisema amefuatilia mashindano waliyopata nafasi ya kushiriki Uturuki amegundua kitu kikubwa kilichowaangusha ni kukosa uzoefu, kujiamini na kutokuwa fiti.

“Tutakuwa wenyeji na kikubwa ni kuhakikisha tunapambana kufanya vizuri kwenye uwanja wetu wa nyumbani, kocha anatakiwa kupata michezo mingi ya kirafiki kabla ya mashindano hayo ili kuwajengea kujiamini na uzoefu.

“Nyota wetu ni bora na wana ushindani lakini bado ni wachanga katika mashindano hasa makubwa na sasa tunatarajia kukutana na nchi nyingi, kocha ajitahidi kuwafundisha mazoezi ambayo yanawaandaa kujiamini, kujituma na kutokuwa na wasiwasi kila wanapokutana na wapinzani,” alisema Mogela.