Mo arudisha shangwe Msimbazi

Muktasari:

Mo Dewji alitekwa asubuhi ya Alhamisi, Oktoba 11, mwaka huu na watu wasiojulikana, wakati akienda kufanya mazoezi ya viungo, kwenye gym iliyopo kwenye hoteli ya Colosseum Oysterbay, usiku wa kuamkia jana alipatikana akiwa salama. Kupatikana kwake akiwa hai ndicho kilichokuwa kilio na dua za mashabiki wa Simba na Watanzania kwa ujumla.

Dar es Salaam. Shangwe, vifijo vimetawala kila kona ya nchi hasa kwa wachezaji, mashabiki wa Simba baada ya taarifa za kupatikana kwa mfanyabiashara Mohamed Dewji ‘MO’ usiku wa kuamkia jana kwenye Viwanja vya Gymkhana Dar es Salaam.

Mo Dewji alitekwa asubuhi ya Alhamisi, Oktoba 11, mwaka huu na watu wasiojulikana, wakati akienda kufanya mazoezi ya viungo, kwenye gym iliyopo kwenye hoteli ya Colosseum Oysterbay, usiku wa kuamkia jana alipatikana akiwa salama.

Kupatikana kwake akiwa hai ndicho kilichokuwa kilio na dua za mashabiki wa Simba na Watanzania kwa ujumla.

Akizungumza muda mfupi baada ya kupatikana, MO kupitia kupitia akaunti ya Twitter ya Kampuni ya Mohamed Enterprise Limited (Metl Group) alisema: “Ninamshukuru mwenyezi Mungu nimerudi salama nyumbani.

“Nawashukuru Watanzania wenzangu na watu wote kote duniani kwa dua na sala zao. Nashukuru mamlaka zote, ikiwemo jeshi la polisi, zilizofanya kazi ya kuhakikisha narudi salama,” alisema MO.

Akithibisha kupatikana kwake Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro alisema waliomteka MO Dewji walitaka kupewa fedha licha ya kutotaja kiwango wanachohitaji.

“Ila MO Dewji amesema waliomteka walikuwa na wasiwasi na walizungumza na baba yake (Gullam Dewji-baba mzazi wa MO Dewji). Pia ameeleza jinsi walivyomchukua pale hotelini (Colosseum) na kumpeleka sehemu ambako walimfungia,” alisema IGP Sirro.

Furaha yarudi Simba

Kaimu Rais wa Klabu ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema jana kuwa wanashukuru Mwenyezi Mungu na wamefurahi kwa MO kupatikana salama.

“Tunamshukuru Mungu, Serikali, wapenda soka, Wanasimba na wananchi wote kwa ujumla kwa dua zao kipindi chote MO akiwa hayupo nasi na mpaka amerudi akiwa salama.

“Niishukuru Serikali imefanya kazi kubwa kuhakikisha kijana wetu anapatikana akiwa salama na sasa tusahau yaliyopita na kuganga yajayo.

Try Again alisema kupatikana kwa MO kumerudisha morali katika timu na anaamini mchezo wa leo dhidi ya Stand United wachezaji watacheza wakiwa na ari kubwa.

“Baada ya taarifa za kupatikana kwa MO niliongea na kocha wetu ambaye aliniambia wachezaji wamefurahi sana leo (jana) na morali yao imepanda kikosini hivyo anaamini hata mashabiki na wanachama wa Simba na kila Mtanzania ana furaha kwa tukio la MO kurudi akiwa salama” alisema Try Again.

Naye Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Hassan Dalali aliyeongoza dua siku aliyotekwa MO alisema: “Wanamshukuru Mwenyezi Mungu amesikia dua zao na MO amepatikana akiwa hai.

“Tunamshukuru Mungu kwa kupokea dua zetu. Mungu alisema ombeni nami nitawapa hivyo amesikia maombi yetu na MO amepatikana. “Tunawashukuru watu wote waliofanya dua kila mahali hapa nchini hadi kijana wetu amepatikana akiwa salama na mwenye afya. Tunashukuru amerejea na kuungana na familia yake na tunatarajia baadae pia ataungana na wanasimba wenzake kuendeleza gurudumu la soka,” alisema Dalali.

Katibu wa Baraza la wazee Simba, Hamisi Kilomoni naye alifanya dua nyumbani kwake kuomba Mungu MO arudi salama.

Beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa alisema anamshukuru Mungu MO amepatikana akiwa salama kwani hilo ndilo kubwa walilokuwa wakimuombea.

“Tulichokuwa tunakipigania na kuomba ni uhai wake, tunashukuru amerudi akiwa salama ili aendelee na kazi zake,” alisema Pawasa.

Wachezaji walipuka kwa shangwe

Mratibu wa klabu ya Simba, Abbas Ally alisema taarifa za kupatikana kwa Dewji ziliwafanya wachezaji walipuke kwa furaha baada ya kuwa katika hali ya sintofahamu kwa siku tisa.

“Ni faraja kwetu wana Simba na wadau wa soka kwa ujumla, mbali kwa wadau na wana Simba, ni faraja pia kwa Watanzania ambao walifanya maombi kumwombea kwa Mungu mara baada ya kutekwa,” alisema Abbas.

Kipa wa Simba, Deogratius Munishi ‘Dida’ alisema hali haikuwa nzuri kwa kipindi chote kwake na wachezaji wenzake tangu Mo Dewji alipotekwa, lakini baada ya kupata taarifa kuwa amepatikana wana amani.

“Ni furaha kubwa kwa sababu ni mtu tunayemtegemea kama unavyojua, sasa akili imetulia kwa sababu awali mambo yalikuwa magumu hata hayo mazoezi tulikuwa tunafanya tufanyeje tu,” alisema Dida.

Wadau walivyofurahia kupatikana Mo

Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Fredrick Mwakalebela alisema kupatikana kwa MO kutaleta chachu ya maendeleo kama vile ambavyo alikuwa akifanya awali.

“MO katika soka si Simba tu bali ni muhimu katika soka la nchi nzima kutokana na anavyofanya au kujitolea katika maendeleo ya soka. Kurudi kwake akiwa mzima ni faraja kwa nchi haswa upande wa michezo,” alisema Mwakalebela.

Kocha msaidizi wa timu ya Taifa ya wanawake Twiga Stars, Edna Lema alisema kurudi kwa MO kumerudisha furaha kwa mashabiki na viongozi wa soka wote hapa nchini.

“Kurudi kwake kutaongeza morali kwa wapenzi wote wa soka hapa nchini haswa wa Simba na hata wachezaji wa klabu hiyo watakuwa katika hali na morali ya kushindana, “ alisema Lema.

Kocha wa makipa wa timu za vijana Tanzania, Manyika Peter alisema watu wote tulikuwa tunaomba arudi salama na imekuwa hivyo tunaomba asiache roho na moyo wake wa kuendeleza michezo licha ya changamoto aliyopata.

Ilivyokuwa baada ya kutekwa

Siku ya tatu tangu kutekwa kwa Mo na watu wasiojulikana, mashabiki wa soka na wakazi wa mikoa mbali mbali nchini walifunguka huku wakimuombea apatikane akiwa salama.

Dewji ‘MO Dewji’ ambaye ni mmiliki wa klabu ya Simba alitekwa wakati akienda kufanya mazoezi ya viungo, kwenye gym iliyopo katika hoteli ya Colosseum iliyopo Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Klabu ya Simba iliendesha kisomo ‘Dua’ maalumu kwenye Makao Makuu ya Klabu hiyo mtaa wa Msimbazi Kariakoo, kwa ajili ya kumlilia na kumuomba Mwenyezi Mungu, amnusuru Mo Dewji aweze kupatikana akiwa hai na salama.

Kisomo hicho kilianza saa 8:00 mchana kwa kuchinjwa mbuzi wawili kwa ajili ya kusindikizia dua hiyo ya kumuangukia Mwenyezi Mungu, kumuomba alisimamie tukio zima la kutekwa kwake.

Mamia ya watu walihudhuria dua hiyo huku maelfu wakiwa nje ya jengo la Makao Makuu ya Klabu hiyo, baadhi ya akina mama wakionekana kujiinamia huku wengi wakibubujikwa machozi muda wote.

Wanariadha wamlilia

Mwanariadha nyota wa zamani na Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi alisema tukio la kutekwa kwa Mo Dewji limewagusa Watanzania wote na sio wanasoka pekee.

Bayi alisema hili ni jambo la kuogopesha na pia linakumbusha umuhimu wa kuwepo tahadhari kwa kwa watu mmoja lakini na vyombo vya usalama kwa ujumla wake.

“Sitaki kulizungumzia sana suala hilo kwani liko chini ya Polisi na matumaini ya kuhakikisha MO anapatikana yapo, lakini hili linatoa funzo gani kwetu? Tujihadhari na maadui kwa kuwa wanatoka mule mule kwa marafiki,” alisema Bayi.

Alisema mtu asijekufahamu hawezi tu kuibuka na kukufanyia tukio la ajabu, lazima anatoka miongoni mwa watu wanaokufahamu vema, hivyo ili kuwa salama ni lazima kuchukua tahadhari mapema,” Bayi ambaye pia ni mmiliki wa shule za Filbert Bayi.

Naye nyota mwingine wa zamani wa Olimpiki na kocha wa timu ya Taifa ya riadha ya Brunei, Sulemain Nyambui alisema tukio hilo ni funzo kwa kila mmoja, licha ya kuwashauri wanariadha hususani wale waliofikia viwango vya kupata fedha nyingi kwenye mbio kuwa waangalifu zaidi.

“Hiyo ni hali hatarishi, lakini naamini kwa uwezo wa Mungu na jitihada za jeshi la Polisi, ndugu yetu huyo atapatikana na niwaombe watu wote wenye fununu za gtukio hili wasaidie kuwaeleza Polisi na vyombo vingine vya usalama ili kuhakikisha anapatikana na wahusika wananaswa na kuchukuliwa hatua, lakini ni wakati sasa wa kuwa waangalifu,” alisema Nyambui kutoka Brunei.

Nyota wa mbio ndefu nchini, Alphonce Simbu alisema tukio hilo limemshtua na linaibua maswali mengi yasiyo na majibu, huku akimuombea MO apatikane na kuungana tena na familia yake.

“Hatukuwahi kufikiria mambo kama hayo, hivi kwa mtu kama MO kutekwa, mchango wake mkubwa ndani ya nchi kwa namna alivyotoa ajira kwa Watanzanai, inabidi kujiuliza mara mbili mbili vipi kuhusu wengine?, cha msingi ni kuchukua tahadhari na tuendelee kumuombea apatikane salama,” alisema Simbu.

Mwanza

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti mashabiki wa soka jijini hapa wengi wao wakiwa na majonzi, walisema tukio hilo ni la kuogopesha lakini kwa kuwa mamlaka zinaendelea kufanya uchunguzi wa tukio zima na kujua aliko wao wanaendelea kumwombea apatikane akiwa hai.

Baadhi ya wanachama hao, Salya Ludanha, Hassan Kaheshi na Juma Mlilo walisema wameumizwa sana na tukio hilo pamoja na vyombo vya dola kuendelea kufanya kazi yake, wao wanaelekeza nguvu zao katika maombi ili mfanyabiashara na mwanamichezo huyo apatikane akiwa hai.

Ludanha ambaye ni Mwenyekiti wa muda wa Klabu ya Simba Mkoa wa Mwanza, aliwaomba mashabiki wa klabu hiyo, wanamichezo na Watanzania kwa ujumla wao kumuombea Mo Dewji apatikane akiwa hai.

“Siwezi kuzungumza zaidi kwa sababu ni mapema ni jambo la kusubiri tu, lakini kikubwa ni kuomba dua ili aweze kupatikana akiwa salama” amesema Kaheshi.

Mkoani Mbeya

Wadau wa soka mkoani Mbeya walisema kitendo cha kutekwa kwa Mo Dewji kinaogofya na ni kitu cha hatari.

Mwenyekiti wa mashabiki wa Simba Mkoa wa Mbeya, John Bondo alisema ‘Inauma sana na kitu ambacho hatukuwahi kukitarajia kama lingetokea hili.

Hapa kwa sasa Watanzania na mashabiki wa Simba tunahitaji kuwa na mshikamano, umoja na kila mmoja wetu azidi kuomba kwa kila aina ya dua kuona kiongozi wetu huko aliko awe salama wakati vyombo vyetu vya usalama vikiendelea na kazi yake,” alisema Bondo.

Katibu Mkuu wa Tanzania Prison, Havintishi Abdalah alisema tukio hilo limeitikisa nchi na Dunia nzima na ni jambo la kuogofia na kusikitisha.

“Hii sio kwa wapenzi wa soka tu ni kwa Watanzania wote.

Inatupa shaka mno. yule ni mtu muhimu sana Tanzania na Afrika nzima Sisi Tanzania Prison, tunaiomba sana Serikali kupitia vyombo vyake vya dola ifanye kazi yake kwa weledi na juhudi mara dufu kuhakikisha anapatikana akiwa hai na salama”.

Havintishi alisema kupitia tukio hilo, Watanzania wanapaswa kudumisha umoja, mshikamano na kutoa ushirikiano wa kila aina kwa Serikali na vyombo vyake vya dola ili kuona Mo Dewji anapatikana na watekaji wanatiwa mbaroni.

MO alitikisa dunia

Kutekwa kwa MO, kulitikisa, si tu Tanzania bali hata anga za kimataifa.

Jarida la Forbes ambalo limekuwa likifanya utafiti wake na kumtangaza mara kwa mara Dewji kama mfanyabiashara kijana aliyefanikiwa zaidi liliandika habari za kutekwa kwake.

Forbes lilisema kuwa Dewji anashika nafasi ya 17 kwa utajiri unaofikia Dola1.5bilion. Vyombo vya habari vya Uingereza, ikiwemo Shirika la Utangazaji, (BBC), Shirika la Habari la Uingereza (Reuters) na baadhi ya magazeti ya; The times, Daily Telegraph, Daily Mail, Irish Times, The Guardian na The Independent yaliandika habari za Dewji kupotea.

Pia habari za MO zilitua Canada ikiwemo gazeti la Ottawacitizen na pia Voice of America, Sauti ya Ujerumani, Kituo cha habari cha Marekani, CNN kilirusha habari za Dewji pamoja na Kituo cha Televisheni cha Al Jazeera cha Qatar kiliandika kwa mapana habari za mfanyabiashara hiyo.