Mo ahitimisha kugawa barakoa

Muktasari:

  • Miongoni mwa vitu ambavyo unatakiwa kuvitumia katika kipindi hiki ili kujikinga na ugonjwa wa covid 19, ambao unaenezwa na virusi vya corona ni kuvaa barakoa, kutokukaa katika mikusanyiko, kunawa kwa sabuni na maji yanayotiririka

TAASISI ya Mo Dewji Foundation wakishirikiana na Simba leo Jumatatu wamehitimisha ugawaji wa barakoa katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Akiwakilisha uongozi wa Simba msaidizi wa Ofisa ya mtendaji mkuu, Rispa Hatibu amesema wamekamilisha zoezi hilo kwa kugawa barakoa  25000.

Rispa anasema zoezi hilo la kugawa barakoa walilihitimisha katika maeneo matatu kuanzia soko la ndizi Mabibo ambapo waligawa barakoa 1000, na baada ya hapo walikwenda masoko mengine ya Tandale na Manzese.

 "Si kama tunagawa barakoa tu bali hata sabuni za maji tumewagawia katika maeneo yote hayo matatu ambayo tulipita na mbali ya kugawa tuliendelea kuhamasisha kujikinga dhidi ya virusi vya corona" alisema Rispa.

Mkuu wa kitengo cha maudhui na mitandao Simba, Rabi Humu alisema zoezi hilo la kugawa barakoa halikuwa kwa mashabiki wa Simba pekee yake bali ni kwa watu wote.

Hume alisema kila waliyemkuta katika eneo husika ambalo walipita walimgawia barakoa bila kujali alikuwa ni shabiki wa timu nyingine.

"Lengo la kugawa barakoa lilikuwa kwa kila mwananchi ambaye atapata aweze kutumia kujikinga na ugonjwa huu wa covid 19, bila kuangalia kama ni shabiki wa Simba au mpenzi wa soka," alisema Rabi.

"Tunashukuru zoezi lilikuwa la kimafanikio kwani barakoa tuligawa zote 25000, lakini hata sabuni ambazo tulikuwa nazo zote tulifikisha kwa walengwa ambao tunaimani watazitumia katika mazingira sahihi," anasema Hume.