Mo aeleza sababu ya kukosa Ligi Kuu

Mshambuliaji Mohamed Rashid ‘Mo’ wa JKT Tanzania amesema sababu kubwa iliyomchelewesha kuonekana katika Ligi Kuu ni majeraha ya nyama za paja aliyoyapata mapema msimu huu.

Hadi sasa, Rashid katika mechi tano hajaonekana katika kikosi hicho tofauti na ilivyokuwa katika msimu uliopita.

Akizungumza jana, mchezaji huyo alisema hakuchana nyama, lakini ulitokea uvimbe katika nyama za paja na hospitali kumshauri apumzike.

“Mara ya kwanza niliumiaga msuli katika mechi dhidi ya Namungo, lakini nikaumia nyama za paja baada ya kupumzika nilivyofanya mazoezi ya baharini kwa nguvu.” alisema.

Akizungumzia hali yake kwa sasa, Mo alisema ameanza kukaa sawa akiwa katika uangalizi mzuri ili kurejea uwanjani kuisaidia JKT Tanzania.

“Nipo kwenye uangalizi wa Dk Gilbert, ameniambia nianze mazoezi polepole na baada ya hapo sasa ndiyo niende nimwambie kama nasikia maumivu katika eneo gani, au kama sisikii maumivu pia niseme,” alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba na Tanzania Prisons.

JKT Tanzania kwa sasa inashika nafasi ya 16 ikiwa na pointi 4 katika mechi tano walizocheza wakishinda mechi moja, sare moja na kupoteza mechi tatu, huku wakifunga mabao mawili na kuruhusu tisa katika michezo mitano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.