Mo Salah, Aubameyang wapangwa chama moja

Thursday January 10 2019

 

DAKAR, SENEGAL.WASHAMBULIAJI watatu wanaoishika Ligi Kuu England kwa sasa, Mohamed Salah, Sadio Mane na Pierre-Emerick Aubameyang wamechaguliwa kuunda safu ya ushambuliaji ya kikosi cha kwanza cha mwaka cha wachezaji wa Afrika.

Mo Salah wa Liverpool ameshinda pia tuzo ya kuwa mchezaji bora wa Afrika kwa mwaka wa pili mfululizo, hivyo kwenye kikosi hicho cha Afrika atajumuika na staa mwenzake wa Anfield, Mane pamoja na fowadi matata wa Arsenal, Aubameyang.

Kikosi hicho kimejaa wanasoka wa kutoka Ligi Kuu England na wengine ni Serge Aurier, Eric Bailly, Naby Keita na Riyad Mahrez, ambao watafiti kwenye mfumo wa 4-3-3.

Salah alifunga mabao 44 Liverpool na Misri mwaka 2018, huku akishinda pia Kiatu cha Dhahabu cha Ligi Kuu England msimu uliopita.

Mane alifunga mabao 20 katika mechi 44, hadi sasa ameshafunga mabao tisa katika mechi 26. Aubameyang ni kinara wa mabao huko Arsenal, akifunga mara 16 katika mechi 26. Aurier, anakipiga kwenye kikosi cha Tottenham naye ameingia kwenye kikosi hicho, huku Eric Bailly wa Manchester United, Riyad Mahrez wa Manchester City na Naby Keita nao wakiwamo kwenye orodha.

Beki wa Napoli, anayewindwa na Man United, Kalidou Koulibaly, naye amepata nafasi sawa na Medhi Benatia wa AS Roma, huku kipa wao ni Denis Onyango wa Uganda.

Advertisement