Mnaijeria achomoka jela baada ya miezi 4

Saturday November 30 2019

By Thomas Ng'itu

KIUNGO wa zamani wa Stand United, Ahmed Adewale Tajudeen, raia wa Nigeria ameachiwa huru baada ya kumaliza kifungo cha miezi sita mkoani Morogoro alikokamatwa akielekea Iringa.

Adewale alikamatwa na Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Morogoro, Julai 17 kwa kosa la kuishi na kufanya kazi nchini bila vibali ambapo alifungwa katika Gereza la Morogoro.

Akizungumza na Mwanaspoti akiwa nchini kwao Nigeria, Tajudeen alisema tukio hilo lilitokana na uongozi wa zamani Stand United kutompatia vibali hivyo.

“Mkataba wangu na Stand ulikuwa unamalizika Julai 25, lakini wao walitakiwa wahakikishe niwe na vibali kwa sababu ndio nilikuwa naitumikia timu yao na mkataba wangu ulikuwa haujamalizika,” alisema.

Alieleza kwamba baada ya Stand kushuka daraja alipata kuzungumza na Lipuli FC kwa ajili ya usajili mpya ndipo alipokamatwa na Uhamiaji alipofika Morogoro.

“Nilipofika Morogoro nilikamatwa na Uhamiaji, nilikuwa naenda kufanya mazungumzo na Lipuli, basi nilishushwa kwenye gari na kuambiwa sina vibali vya kuishi, lakini yote haya ni Stand ndio wamenifanyia kwa sababu sikuwa na vibali vya kuishi muda wote.”

Advertisement

Kiungo huyo alisema baada ya kukamatwa hakuwa na jinsi zaidi ya kwenda kutumikia kifungo. “Niko nyumbani nimejigharamia nauli mwenyewe na nimefanikiwa kurudi, shukrani kwa mchezaji mwenzangu wa Stand ambaye alikuwa anakuja kuniona tangu nimekamatwa, na wote ambao walikuwa wakimpa michango yao Elias kwani ilikuwa ikifika vizuri,” alisema.

Tajudeen alisema kwa kipindi hiki hana mipango ya kurejea tena nchini kwani anataka kutuliza akili baada ya misukosuko ambayo amepitia.

“Misukosuko niliyopitia lazima nitulize akili kidogo, nadhani nahitaji kwenda sehemu nyingine kucheza na hata kama nitarudi Tanzania basi itakuwa ni mwakani.”

Advertisement