Mmoja nje Serengeti Boys

Muktasari:

  • Chanzo kilicholidokeza Mwanaspoti, kilisema mchezaji huyo tayari ameshaondolewa na hayupo katika mipango ya kocha licha ya kwamba alikuwa katika kikosi cha awali.

KIKOSI cha Timu ya Taifa ya Vijana U-17, Serengeti Boys kipo kwenye maandalizi ya kwenda kuweka kambi Qatar, lakini huku nyuma ikidokezwa mmoja wa nyota wake amechomolewa.

Nyota huyo, Amiri Njeru aliyekuwa kwenye kikosi kilichoshiriki michuano maalumu ya UEFA Assist kule Uturuki amechomolewa kimyakimya kwa utovu wa nidhamu.

Kilichomponza kinda huyo ni video iliyosambaa mitandaoni, ambapo Njeru alionekana akiwasifia wapinzani wao kuwa ni bora baada ya kucheza nao katika michuano hiyo ya U-17.

Inatajwa baada ya kurejea nchini mmoja wa vigogo ndani ya TFF aliwataka wachezaji hao wahojiwe kwanini walijirekodi video ile na waliposikilizwa Njeru ndio alitolewa.

Chanzo kilicholidokeza Mwanaspoti, kilisema mchezaji huyo tayari ameshaondolewa na hayupo katika mipango ya kocha licha ya kwamba alikuwa katika kikosi cha awali.

Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Ammy Ninje alitafutwa ili afafanue mkasa wa Njeru, lakini ilishindikana kwa kuwa kila simu yake ilipopigwa haikuwa ikipatikana na alipotafutwa kwa njia ya Whatsapp alijibu ujumbe kuwa yupo Uingereza.