Mlandege wampa Ame kumbukumbu

Saturday October 17 2020

 

By Charles Abel

Beki wa kati wa Simba, Ibrahim Ame kwa mara ya kwanza leo Oktoba 17, 2020 amefunga bao akiwa na jezi za timu hiyo katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Mlandege ambao unachezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini.

Bao hilo la Ame amelifunga katika dakika ya 16 ya mchezo akiunganisha kona ya Luis Miquissone.

Kona hiyo iliyozaa bao ilitokana na mpira uliookolewa vibaya na mmoja wa walinzi wa Mlandege wakati alipokuwa katika jitihada za kuokoa shambulizi la Miquissone.

Tangu alipojiunga na Simba akitokea Coastal Union katika dirisha kubwa la usajili mwezi Agosti, Ame alikuwa hajawahi kufunga bao lolote akiwa na jezi ya Simba katika mechi za kirafiki na zile za mashindano.

Kabla ya bao hilo la Ame, Simba ilitangulia kupata bao la kuongoza kupitia kwa Chris Mugalu.

Hilo ni bao la tano kufungwa na Mugalu katika mechi tano alizoichezea timu hiyo, akifumania nyavu katika kila mchezo waliocheza dhidi ya timu za Vital'O, Biashara United, Gwambina FC, JKT Tanzania na leo dhidi ya Mlandege.

Advertisement

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Simba inaongoza kwa mabao 2-0 huku ikiwa imetengeneza nafasi nyingi ambazo hazijamaliziwa vyema na washambuliaji wao.

Advertisement