Mkwasa arejesha furaha Yanga, KMC mambo bado magumu

Friday November 8 2019

 

By Thomas Ng'itu

BAO la Patrick Sibomana limeifanya Yanga kuibuka kidedea kwa ushindi wa 1-0 katika mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Ndanda uliochezwa katika uwanja wa Nangwanda Sijona, Mtwara, ikiwa mechi ya kwanza chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Boniface Mkwasa aliyemrithi Mwinyi Zahera.
Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha pointi 10 na kuchupa hadi nafasi ya 14 wakimshusha  Azam ambao usiku huu wanajiandaa kuvaana na Biashara Utd katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu.
Katika mchezo huo  Ndanda walicheza kwa kuonyesha nidhamu kwa Yanga, huku wakifanya mashambulizi ya kushtukiza wakiwa wanatafuta namna ya kuingia katika safu ya ulinzi ya Yanga iliyokuwa inoangozwa na Kelvin Yondani.
Washambuliaji wa Ndanda wakiongozwa na Hussein Javu walikuwa wakifosi kuingia ndani ya boksi lakini walikuwa wakikumbana na changamoto kutoka kwenye safu ya ulinzi.
Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza hakukuwa na timu yoyote ambayo iliweza kupata goli la kuongoza  katika mchezo huo.
Katika kipindi cha pili Yanga walionekana na kuonyesha Dhahiri wanahitaji goli baada ya kutengeneza nafasi za  mfululizo langoni mwa Ndanda Fc.
Dakika 51  Yanga ilitaka kupata bao kupitia kwa winga wake Deus Kaseke ambaye alimtoka beki wa Ndanda, Paul Maona na kupiga shuti lilitoka juu kidogo ya mwamba.
Ndanda walifanya mabadiliko dakika 65 kwa kumtoa Hussei Javu na kuingia Nassor Saleh  wakati huo huo Yanga wakifanya mabadiliko ya kumtoa Rafael Daud na kuingia Mrisho Ngassa.
Yanga ilipata goli dakika 75 kupitia kwa faulo iliyopigwa moja kwa moja wavuni baada ya beki wa Ndanda, Aziz Sibo kuunawa mpira nje kidogo ya boksi.
Dakika 88 Ndanda ilishtua kidogo baada ya kumtoa mchezaji Nassor Saleh ambaye aliingia akichukua nafasi ya Hussein Javu, Nassor alitoka tena na nafasi yake ilichukuliwa na Yasin Mohamed.
KMC NGOMA NGUMU
Kwa upande wa klabu ya KMC hali yao bado ni tete licha ya kutaka kujiinua baada ya kuanza kuweka figisu ya kumtema kocha wao mkuu, Jackson Mayanja.
Mayanja katika mchezo huu pia aliendelea kukosekana kwa madai ya kukosa vibali vya kufanyia kazi nchini, kocha huyo alianza kukosekana katika mchezo uliopita dhidi ya Biashara Utd na nafasi yake alikaa kocha msaidizi Mrage Kabange.
Katika mchezo wao uliopigwa leo katika uwanja wa Uhuru, KMC wamefungwa 2-1 na Kagera Sugar ambayo katika mchezo wao uliopita walitoka sare 0-0 na Azam.
Magoli ya Kagera Sugar yalifungwa na Awesu Awesu kwa mkwaju wa penalti dakika 25 na goli la pili lilifungwa na Peter Mwalyanzi dakika 45 huku lile la kufutia machozi likifungwa na Serge Alain dakika 87.

Msimamo wa Ligi Kuu Bara 2019-2020
        P    W    D    L    F    A    PTS
1. Simba        9    7    1    1    16    3    22
2. Kagera Sugar    10    6    2    2    14    8    20
3. Tanzania Prisons    10    3    7    0    11    7    16
4. Namungo FC    10     5    1    4    9    8    16
5. Lipuli FC    9    4    3    2    13    9    15
6. JKT Tanzania    10    4    3    3    8    8    15
7. Mtibwa Sugar    11    4    3    4    10    11    15
8. Ruvu Shooting    11    4    3    4    9    10    15
9. Alliance FC    10    3    5    2    8    7    14
10.Mbao FC    11    3    5    3    9    9    14
11.Polisi Tanzania     9    4    1    4    9    10    13
12. Coastal Union    10    3    2    5    8    9    11
13.Mwadui FC    11    2    5    4    7    10    11
14.Yanga        5    3    1    1    6    4    10
15.Azam FC    6    3    1    2    5    3    10
16.KMC FC    8    2    2    4    5    8    8
17.Biashara United    9    2    2    5    5    9    8
18.Mbeya City    10    1    5    4    7    16    8
19.Ndanda FC    9    1    4    4    6    9    7
20.Singida United    10    0    4    6    3    10    4
* Kabla mechi ya usiku huu kati ya Azam na Biashara United

WAFUNGAJI
8 Meddie Kagere (Simba)- Rwanda
6 Daruesh Seif Saliboko (Lipuli)
    Paul Nonga (Lipuli FC)
4 Athuman Miraj (Simba)
   Peter Mapunda (Mbeya City)
   Yusuf Mhilu (Kagera Sugar)
   Gerald Mathias Mdamu (Mwadui)

Advertisement