Mkwasa amaliza ubishi fasta

Muktasari:

Yanga katika michezo yake mitano kwenye Ligi Kuu, imeibuka na ushindi mara tatu na kutoka sare mbili huku ikifunga jumla ya mabao manne na kuruhusu nyavu kutikiswa mara tatu.

KATIKA mechi kali na ambayo shabiki wa mpira hupaswi kuikosa leo Jumanne ni ule wa Polisi Tanzania dhidi ya Yanga mjini Moshi kwenye Uwanja wa Ushirika. Lakini Kocha Msaidizi wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa ametamka liwalo na liwe lazima washinde ili kuonyesha nia yao ya kuutaka ubingwa, ingawa Polisi wamesikia wakajichekea tu.

Stresi ambazo timu hizo zimepata kutokana na matokeo ya mechi zilizopita, huenda zikachangia utamu zaidi kwenye kiwango cha soka katika mchezo wa leo.

Polisi Tanzania inarudi nyumbani baada ya kucheza mechi tano mfululizo ugenini ambako imepata ushindi mara mbili dhidi ya JKT Tanzania na KMC na kupoteza tatu nyingine dhidi ya Azam FC, Simba na Coastal Union huku ikifunga mabao matano na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara saba.

Yanga katika michezo yake mitano kwenye Ligi Kuu, imeibuka na ushindi mara tatu na kutoka sare mbili huku ikifunga jumla ya mabao manne na kuruhusu nyavu kutikiswa mara tatu.

POLISI WABABE

Polisi Tanzania wamekuwa na rekodi nzuri dhidi ya Yanga kwani katika mechi mbili imepata ushindi mara moja na kutoka sare mara moja. Ilipata ushindi katika mchezo wa kirafiki Agosti 16 mwaka jana katika Uwanja wa Ushirika Moshi mkoani humo lakini pia zilikutana tena katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu Uwanja wa Uhuru jijini na kutoka sare ya mabao 3-3.

Maafande hao ambao wanashika nafasi ya 10 wakiwa na pointi 29 wamekuwa wakitumia mbinu ambazo zimekuwa zikiwapa shida mara kwa mara wapinzani wao. Mbinu yao kubwa ambayo wamekuwa wakiitumia ni ile ya wachezaji wake kujazana kwa idadi kubwa nyuma ya mstari unaougawa uwanja katika eneo lao kisha kuingia kwa haraka katika upande wa adui pindi wanapounasa mpira.

YANGA WAMEJIPANGA

Polisi wanapaswa kuwa makini zaidi na mbinu za Yanga chini ya Kocha Luc Eymael ikiwa ina nia ya dhati ya kupata matokeo mazuri. Nguvu kubwa ya Yanga ipo katikati ya uwanja na imekuwa ikiwategemea zaidi viungo Haruna Niyonzima, Papy Tshishimbi na Mapinduzi Balama katika kutawanya mipira pembezoni mwa uwanja hasa upande wa kulia ambako ndiko hutumika kuzalisha mabao.

Uwezo na ufanisi wa viungo hao ndio umekuwa ukiisaidia Yanga kuwalazimisha mabeki na viungo wa timu pinzani kuachia mianya ambayo ndio huitumia kutengeneza mabao yake.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Charles Mkwasa, alisema wanatambua ugumu wa Polisi Tanzania, kwakuwa waliwasumbua katika mchezo uliopita, lakini hawatakubali kupoteza au kuambulia alama moja kwa mara ya pili katika mchezo huo.

“Mchezo wa kwanza tukiwa nyumbani tulikubali sare ya bao 3-3 kama wao waliweza kutufunga kwenye uwanja wetu sisi pia tunaweza kupata matokeo ugenini mbinu na maandalizi ndio yatakayoamua matokeo na sio uwanja,” alisema Mkwasa ambaye ni staa wa zamani wa Yanga.

“Tunakutana na timu ambayo imetoka kupata matokeo mazuri na sisi tumetoka kuambulia sare nyumbani hivyo tunatarajia mchezo wa ushindani kutokana na kila timu kuhitaji matokeo na kujiimarisha kwenye msimamo wa ligi ukiwa ni mzunguko wa lala kwa usalama,” alisema Mkwasa. Wapo nyota ambao kwa namna moja au nyingine kila upande unapaswa kuwachunga zaidi ili wasilete madhara kwao.

Nyota wanaopaswa kuchungwa zaidi upande wa Yanga ni Bernard Morrison, Niyonzima na Nchimbi wakati kwa upande wa Polisi Tanzania ni Marcel Kaheza, Pato Ngonyani na Sixtus Sabilo kutokana na kiwango bora ambacho wamekuwa wakikionyesha katika mechi za hivi karibuni na ndio wamekuwa wakitoa mchango mkubwa kwa timu hizo.

MAJOGORO

Kiungo wa Polisi Tanzania, Baraka Majogoro alisema Yanga ya mzunguko huu imebadilika tofauti na mzunguko wa kwanza lakini hilo haliwazuii kupata matokeo. “Mechi itakuwa ngumu zaidi tofauti na mzunguko wa kwanza Yanga imefanya usajili katika nafasi mbalimbali, lakini tunatakiwa kupambana ili kuendelea kuwashawishi mashabiki wa Polisi kuendelea kuisapoti timu,” alisema.