Mkwasa alia na mabadiliko ya viwanja

Muktasari:

Ruvu Shooting inashika nafasi 10 ikiwa na pointi 5 tu katika mechi nne walizocheza mpaka sasa.

KOCHA Mkuu wa Ruvu Shooting, Charles Mkwasa ameweka wazi hali ya kubadilishiwa uwanja, umeathiri kikosi chao katika mchezo dhidi ya Biashara Utd uliomalizika bila kufungana.

 Ruvu Shooting inatumia Uwanja wa Mabatini kama uwanja wa nyumbani, lakini ni miongoni mwa viwanja vitano ambavyo hivi karibuni vimefungiwa na Bodi ya Ligi baada ya kutokuwa na vigezo mbalimbali.

 Akizungumza na Mwanaspoti Online leo Jumanne Septemba 29, 2020, Mkwasa amesema kisaikolojia kubadilishwa uwanja iliwaathiri katika mchezo huo lakini washambuliaji wake nao wamemuangusha.

 "Washambuliaji hawajatumia nafasi vizuri ambazo tumetengeneza licha ya kwamba mazoezini wanafanya vizuri, mchezo ulikuwa mgumu na tunajipanga na mchezo mwingine" amesema

 Naye kocha wa Biashara Utd, Francis Baraza aliwapongeza wachezaji wake kwa kucheza vizuri katika mchezo huo hasa kufuata mambo aliyokuwa anayahitaji.

 "Nilikuwa nataka viungo wangu washuke chini waje kuchukua mipira na kisha kusambaza na jambo hilo tulifanikiwa, kiujumla mchezo ulikuwa mzuri na katika mchezo wao wa mwisho wapinzani wetu walikuwa bora" amesema Baraza.