Mkwasa,Manyika wajilipua Yanga

KOCHA Charles Mkwasa ametoboa namna walivyofanya kazi na kocha mkuu, Luc Eymael kabla ya kutimuliwa kutokana na matamshi yake ya kibaguzi.

Mkwasa kocha msaidizi wa Yanga amesema kuwa: “Tulijaribu kumsaidia, lakini hasaidiki.”

Kocha huyo aliyewahi pia kuwa mchezaji na katibu mkuu wa Yanga kwa nyakati tofauti aliyasema hayo katika mahojiano na Mwanaspoti.

“Mambo mengi yalikuwa hayaendi, tulivumilia vingi, ilifikia mahali timu ilikuwa inapoteza mwelekeo, lakini tunashindwa kusema sababu tungeonekana tunamchongea.

“Lakini mwisho wa siku ukweli umeonekana,” alisema Mkwasa akisisitiza kuwa kocha huyo amenusurika mara kadhaa kupewa kadi nyekundu akiwa kwenye benchi kutokana na matamshi yake.

“Tulikuwa tukiwaomba waamuzi watusamehe sisi kutokana na matamshi yake kwao, lakini kama ni kadi nyekundu angeshapewa siku nyingi.”

Kocha wa makipa wa Yanga, Peter Manyika ambaye kuna tetesi alitaka kuzichapa na Eymael alisema hayupo katika nafasi ya kuzungumzia sakata hilo kwa undani.

“Uongozi unafahamu kila kitu kuhusu tulivyoishi na kocha mkuu (Eymael), hivyo wao ndiyo watakueleza ipasavyo kwani muda mwingi wakati tunatofautiana naye, Bumbuli (ofisa habari wa klabu) alikuwepo,” alisema.

Bumbuli alipoulizwa alisema klabu yao sasa inasonga mbele, imeachana na habari za Eymael ambaye alidai alikuja kuinoa Yanga kwa bahati mbaya.

Yanga ilimfuta kazi Eymael Julai 27 na kumtaka kuondoka nchini haraka kwa kutoa kauli ya kibaguzi, ingawa kocha huyo alikaririwa na gazeti hili juzi akisema yeye si mbaguzi wa rangi.