Mkwasa: Niko fiti hata soka napiga

Muktasari:

Akizungumza na Mwanaspoti akiwa Mtwara na Yanga inayojiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ndanda, nyota huyo wa zamani wa kimataifa alisema kwa mujibu wa daktari wake aliyemtibia India alimpa mapumziko ya miezi sita ambayo ameshaikamilisha, hivyo anaruhusiwa kuendelea na majukumu yake.

UTEUZI wa Charles Boniface Mkwasa kuwa kocha mkuu wa muda wa Yanga, ikiwa ametoka kufanyiwa upasuaji wa moyo kule India, kumeibua maswali kwa baadhi ya wadau, lakini mwenyewe amefichua kuwa yupo fiti kinoma kiasi hata kucheza mpira anaweza kukinukisha freshi tu.

Mkwasa aliyejiuzulu ukatibu mkuu tangu Februari Mosi, 2017 kwa matatizo ya kiafya kabla ya kwenda kufanyiwa upasuaji India alikuwa nje ya soka kwa muda mrefu, lakini amefichua kwa sasa yupo fiti, hivyo haoni kama kuteuliwa kwake kuwa kocha wa Yanga ni tatizo kwani hata kukiwasha anaweza.

Akizungumza na Mwanaspoti akiwa Mtwara na Yanga inayojiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ndanda, nyota huyo wa zamani wa kimataifa alisema kwa mujibu wa daktari wake aliyemtibia India alimpa mapumziko ya miezi sita ambayo ameshaikamilisha, hivyo anaruhusiwa kuendelea na majukumu yake.

“Nilipewa mapumziko ya miezi sita tangu Mei mwaka huu niliporudi tena India kwenye matibabu ya mwisho niliambiwa naweza kucheza hadi soka kwa namna nilivyohudumiwa, hivyo niko fiti sihofii lolote kwenye hilo.

“Nimefanya kazi Yanga nikiwa kama kiongozi, kocha na nimeichezea hivyo presha ya timu hii naifahamu na najua namna ya kuikabili sina wasiwasi wowote kikubwa nahitaji ushirikiano tu,” alisema.

Akizungumzia suala la kutoka kuwa katibu mkuu hadi kuiongoza Yanga kama kaimu kocha, Mkwasa alisema uongozi sio kipaumbele chake na kitu kikubwa alichokitamka hata alivyokuwa anaumwa kama atapewa uhai zaidi kitu ambacho anaweza kukifanya ni ukocha na sio uongozi.

“Kuongoza watu inahitaji moyo na kukubaliana na kila kitu, hilo kwangu sio kipaumbele ninachoweza kufanya ni kufundisha na namshukuru Mungu nimepata nafasi hiyo nitaendelea kufanya hivyo,” alisema.

KAULI YA KWANZA KWA WACHEZAJI

Mkwasa alidokeza muda mchache baada ya kuteuliwa kukaimu nafasi hiyo kitu kikubwa alichowaambia wachezaji ni kuhakikiha kila mmoja wao anakuwa na lengo moja la kuona timu inatwaa taji la Ligi Kuu.

Mkwasa amekaimu nafasi hiyo baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera kufungashiwa virago kutokana na kushindwa kufikia malengo ya klabu.

Mkwasa alisema ni lazima waanze kushinda mechi zao huku akiwaambia nyota wake wakitaka wasichukiwe na mashabiki watimize wajibu wao.

“Hamtachukiwa na mashabiki kama mtacheza vizuri na kushinda, maisha yenu yatakuwa mazuri sana, Wanayanga watajitokeza kwa wingi uwanjani na mtalipwa kwa wakati stahiki zetu,” alisema.

“Nyinyi ni wachezaji wazuri sana na mimi niko hapa kuwasaidia kufanikisha hilo ninachokitaka kutoka kwenu ni ushirikiano wa hari na mali ili tuweze kulisongeza gurudumu salama na kufikia mafanikio naamini hili linawezekana,” alisema.

Kwenye hilo la Yanga, amebaki Kocha wa Makipa Peter Manyika tu.