Mkude ashtukia mazoezi ya kila mtu kivyake janga kwa Simba SC

Muktasari:

Simba ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara na ndio timu inayoongoza kwa pointi ikiwa ya kwanza kwenye msimamo baada ya kufanikiwa kujikusanyia pointi 71

KIUNGO wa Simba, Jonas Mkude amesema endapo Ligi Kuu Tanzania Bara itaendelea kutakuwa na changamoto mbalimbali kwa wachezaji kurejea katika ari ya mchezo.
Jambo ambalo Mkude analiona litakuwa gumu zaidi ni uwiano tofauti wa pumzi kutokana na kila mtu kufanya mazoezi kivyake na kwamba, haamini kama kila mchezaji anajibidiisha.
Ligi duniani kote zimesimama kupisha janga la ugonjwa wa corona ambao umekuwa changamoto na kusababisha mambo mengi kusimama.
Mkude alisema: “Mazoezi ya kujitenga kila mmoja yana manufaa kwa kila mchezaji, kwa timu sina hakika kwenye hilo kwani ugumu ni pale tutakapokutana na kila mmoja kuwa na pumzi tofauti maana kutakuwa na waliokuwa wanajituma sana na waliokuwa wanategea.
“Kikubwa ninachoweza kusema tutakutana na ugumu na itakuwa ni changamoto kwetu kwani tumeachana tukiwa tumetoka katika muunganiko mzuri na tupo fiti kwa upambanaji, sidhani kama tutarudi hivyo,” alisema.
Mkude aliongeza kuwa ni imani yake kila mchezaji aliyepo nyumbani anajitambua na anatambua kuwa kuna ligi bado itaendelea, hivyo alitumia nafasi hiyo kuwashauri kufanya mazoezi kwa wakati ili wakirudi waendeleze kasi na kufikia malengo.
Simba ndio mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara na ndio timu inayoongoza kwa pointi ikiwa ya kwanza kwenye msimamo baada ya kufanikiwa kujikusanyia pointi 71. Kwa sasa mastaa wa timu hiyo wako majumbani kwao.