Mkopo wanukia kwa Mesut Ozil Januari

Muktasari:

Ozil atatimiza umri wa miaka 31 wiki ijayo na anajua atalazimika kwenda kwingine kwa ajili ya kupata nafasi ya kudumu katika dirisha la Januari.

ARSENAL ipo katika mazungumzo na Klabu ya Fenerbahce ya Uturuki kwa ajili ya kuipa staa wake wa kimataifa wa Ujerumani, Mesut Ozil, 30 kwa uhamisho wa mkopo huku Arsenal ikiendelea kulipa sehemu ya mshahara wake mkubwa wa Pauni 350,000 kwa wiki.

Kocha wa Arsenal, Unai Emery amemuondoa Ozil katika mipango yake na amependelea zaidi kuwapanga makinda klabuni hapo huku ikiaminika kwamba anataka kuachana na staa huyo katika dirisha la Januari.

Ozil atatimiza umri wa miaka 31 wiki ijayo na anajua atalazimika kwenda kwingine kwa ajili ya kupata nafasi ya kudumu katika dirisha la Januari.

Kwa ujumla, Ozil amecheza mchezo mmoja tu wa Ligi Kuu England katika msimu huu, akiingia dhidi ya Watford ambao uliisha kwa sare ya mabao 2-2. Kocha Emery amekuwa akiwapa nafasi zaidi makinda Dani Ceballos na Joe Willock kufanya majukumu ya kucheza kwenye nafasi ya Namba 10.