Breaking News
 

Mkongomani Yanga arudishwa Dar fasta

Thursday January 11 2018Kocha Mkuu wa timu hiyo, George Lwandamina

Kocha Mkuu wa timu hiyo, George Lwandamina 

By KHATIMU NAHEKA

MASHABIKI wa Yanga mpaka sasa hawajui lolote kuhusu beki wao wa kati kutoka DR Congo, Fiston Kayembe, kwani hajajiunga na timu hiyo tangu aliposajiliwa kwa mkataba wa miaka miwili Novemba mwaka jana.

Lakini minong’ono ya chinichini ya wanachama na mashabiki wa Jangwani kumbe imemfikia Kocha Mkuu wa timu hiyo, George Lwandamina, ambaye amewaambia mabosi wa timu hiyo kwamba anamtaka beki huyo Dar es Salaam fasta.

Lwandamina ametaka beki huyo Mkongomani aliyependekezwa na kiungo Papy Kabamba Tshishimbi, atue nchini kabla ya kuendelea kwa mechi za Ligi Kuu Bara.

Akizungumza na Mwanaspoti, Lwandamina alisema aliposikia Kayembe bado hajajiunga na timu hiyo alilazimika kukutana na vigogo wa Kamati ya Mashindano na kufanya nao kikao kifupi kufahamu kilichomchelewesha beki huyo.

Lwandamina alisema baada ya kuridhishwa na majibu ya mabosi hao, aliwataka kuchangamka na kuhakikisha anarejea nchini kabla ya Ligi Kuu haijaendelea mwishoni mwa wiki hii ingawa Yanga itacheza katikati ya wiki ijayo dhidi ya Mwadui.

Mzambia huyo aliyewahi kuzinoa Mufulira Wanderers na Zesco United za kwao Zambia, alisema anataka kuanza mapema kazi ya kusuka kikosi cha Ligi ya Mabingwa Afrika na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, hivyo anataka kuona kila mchezaji anahusika.

“Niliuliza hata mimi juu ya kwanini mpaka sasa hajawasili, lakini viongozi wameaniambia sababu na nimeelewa, nafikiri watafanya kama ambavyo

tumekubaliana,” alisema Lwandamina.

“Kayembe, ni mmoja wa wachezaji wa Yanga na huu ulikuwa wakati mzuri wa kuwa na wenzake, tukimaliza Kombe la Mapinduzi tutakuwa katika mikakati mikubwa ya kutengeneza kikosi ndiyo maana nimewaambia kabla ya kuendelea kwa ligi anatakiwa awe hapa.”

Beki huyo aliyekuwa akiichezea SM Sanga Balende ya kwao DR Congo, alisajiliwa na Yanga kwenye dirisha dogo, lakini alitimkia kwao kufuatilia vibali vyake na kulikuwa na ukimya juu ya kurejea kwake nchini wakati wenzake wakipiga kazi.

Hali hiyo ndio iliyozua wasiwasi kwa mashabiki kwa kudhani dili lake la kutua Jangwani limekwama.