Mkongo Yanga aamua kukausha

Muktasari:

  • Baadhi ya waliotajwa kutaka kutemwa ni pamoja na nyota wa kimataifa Amissi Tambwe na Thabani Kamusoko sambamba na nyota wengine sita wazawa waliopangwa kutolewa kwa mkopo.

WAKATI kikosi cha Yanga kikiendelea na maandalizi kwa ajili ya mechi zao mbili za viporo Kanda ya Ziwa, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mwinyi Zahera amewafanyia sapraizi mashabiki wa klabu hiyo kwa kuamua kuwakaushia baadhi ya nyota wake.

Zahera aliyepo kwao na kikosi cha timu ya Taifa ya DR Congo anayoinoa kama kocha msaidizi, amesema kwa hali inayoendelea ndani ya Yanga ni dhahiri inaweza kukwamisha mpango yake ya kuwatema baadhi ya nyota ambao, hakutaka kuendelea kuwa nao kwenye duru la pili la Ligi Kuu Bara.

Baadhi ya waliotajwa kutaka kutemwa ni pamoja na nyota wa kimataifa Amissi Tambwe na Thabani Kamusoko sambamba na nyota wengine sita wazawa waliopangwa kutolewa kwa mkopo.

Hata hivyo, Zahera aliliambia Mwanaspoti kuwa, anashindwa kufanya maamuzi kwa sasa ya kuwatoa kwa mkopo wachezaji ambao, hawakuwa na mchango mkubwa ndani ya kikosi hicho kutokana na hali ya ukata uliopo.

Alitoa sababu ya kauli yake kuwa, anaona hali ya kiuchumi bado haijatengemaa ndani ya timu hiyo na kupelekea kuwa na wasiwasi wa kuona mipango yake kabambe ya kutema na kusajili wachezaji inaweza isifike mwisho ingawa alikiri muda bado, lakini kujihami ndio akili.

“Kwa sasa nitatawaliwa na kimya cha wachezaji gani ninaweza nikawaacha kwani, ngumu kuwatema kama itakosekana pesa ya kuwaleta wale ambao, wataziba mapengo yao kupitia usajili wa dirisha dogo.

“Nilifanya zoezi la kuwapatia viongozi majina ya wachezaji ninaowahitaji na wanaotakiwa kuachwa, lakini siwezi kuwalazimisha wakati najua hali halisi ya timu ilivyo kwa sasa, naamini wanapambana ndio maana naendelea kusubiri.”

AWAJAZA UPEPO MASHABIKI

Zahera pia aliamua kuwajaza upepo mashabiki kwa kuwataka wajifunze kujitoa kwa hali na mali kwa klabu zao wanazozipenda kuliko kutoa kasoro ambazo hawajua nini kinawakabili wachezaji nje ya uwanja.

“Tujaribu kuwaweka karibu wachezaji, pia mashabiki wajue kuwa wachezaji wanakabiliwa na changamoto, mimi napambana kuwatuliza na ndio maana timu inapata matokeo,” alisema Zahera.

MSIKIE NYIKA

Mwanaspoti lilimsaka Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Yanga, Hussein Nyika ili aweze kuzungumzia changamoto hiyo naye alisema muda wa dirisha la usajili haujafika, ila ukifika watafanya kama walivyoagizwa na Zahera.

“Dirisha la usajili bado halijafunguliwa, tuko bize kuiandaa timu iweze kupata matokeo katika michezo yote iliyobaki na muda wa usajili ukifika tutasajili kwa maelekezo ya kocha. Kuhusu ukata katika timu hiyo ni ishu nyingine baina ya timu na viongozi hatuwezi tukakwambia sasa tuna fedha au la,” alisema Nyika.