Mkomola aibana Yanga, Kakolanya bado

Monday December 10 2018

 

By Thomas Ng'itu

WAKATI straika chipukizi wa Yanga, Yohana Mkomola akiiburuza klabu hiyo ofisi za Shirikisho la Sokla Tanzania (TFF), lakini ile barua ya kipa Beno Kakolanya ya kuvunja mkataba imeyeyuka.

Wiki iliyopita inaelezwa Kakolanya aliuandikia Yanga uongozi na kuiwasilisha TFF ili kuvunja mkataba na klabu hiyo, lakini jana Jumapili wakati wachezaji kadhaa wakiziburuza klabu zao ili kuvunjiwa mikataba akiwamo Mkomola imeelezwa barua hiyo haipo TFF.

Jana Jumapili katika ofisi zaTFF kulikuwa na kikao maalumu cha wachezaji waliopeleka madai kwa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, lakini Kakolanya na hata meneja wake, Seleman Haroub hawakuonekana kabisa.

Mwanaspoti lilimdodosa mmopja wa wajumbe waliokuwa wanaendesha kikao hicho, Herman Kidifu, ambaye alisema hawajapokea barua ya madai kutoka kwa Kakolanya.

“Hakuna barua yake iliyofika hapa dhidi ya Yanga, madai yaliyowahi kufika hapo ya mchezaji huyo ni msimu uliopita alipokuwa akiidai klabu yake milioni 11 na alishalipwa,” alisema.

Kakolanya aliposakwa kuulizwa barua yake kutoonekana katika Ofisi za TFF, alisema suala hilo alimuachia meneja wake, ila kwa upande wake alipeleka barua yake makao makuu ya Yanga.

“Kuna kipengele katika mkataba wangu kinaniruhusu kuandika barua ya kuwakumbusha waajiri wangu kuhusu madai yangu ndani ya siku 14 kabla mkataba haujavunjwa, ndio maana nikaandika barua na nikaipeleka na imesainiwa kuwa imepokelewa, hiyo barua inatakiwa kutoa kauli ndani ya hizo siku ndio maana nilianza na uongozi wangu,” alisema Kakolanya.

MKOMOLA AKOMAA

Katika kikao hicho cha jana Mwanaspoti liliwashuhudia wachezaji Awadh Salum na Adam Omary wa Africans Lyon, Charles Ilamfya (Mwadui), Yohana Mkomola (Yanga), Babu Ally na Haruna Shamte (Mbeya City) walikuwa wakifuatilia ishu zao ofisi hizo za TFF.

Alipoulizwa kuhusu wachezaji hao, Kidifu alisema kila mmoja ana kesi yake tofauti, ila wachezaji Babu na Shamte wapo huru sasa baada ya pande mbili kukubaliana.

“Hawa wengine bado kesi zao hazijamilika kutokana na kuwapo barua ambazo zinahitajika ili kesi zao ziweze kupata ufumbuzi sahihi kwahiyo bado zinaendelea hazijaishia hapa.”

Hata hivyo, aliongeza upande wa Yohana na Yanga, kuna vuta ni kuvute kwani mchezaji huyo anataka kuvunja mkataba, timu hiyo ikisisitiza haipo tayari kuona hilio linatokea.

“Yohana anatakiwa aandike kwanza barua ya madai kwa uongozi wa klabu yake kisha hayo mambo ya kuvunja mkataba ni mengine ambayo yanakuja baadaye kwahiyo kesi bado,” alisema Kidifu.

Mwanaspoti linafahamu Mkomola amepata dili la nje, lakini Yanga haitaki kuvunja mkataba, bali inataka kumpa barua (Release Letter) kitu ambacho kimeibua vuta nikuvute.

Mwanaspoti likiwa bado katika ofisi hizo, kuliibuka sintofahamu kati ya mmiliki wa African Lyon, Rahim Kangezi na Awadh Salum, kwani mchezaji huyo alisikika akimhoji bosi huyo kwa nini hataki kumuachia wakati alishavunja mkataba wao.

“Nipe barua yangu niondoke sitaki matatizo na wewe, sitaki kucheza katika timu yako si hujanilipa mishahara yangu miezi minne, niache niondoke ili niwe huru,” alisema kiungo huyo aliyefunga bao la kideo siku timu yake ikilala mabao 2-1 mbele ya Simba.

Aidha kiungo huyo alisema yuko tayari kutoa hela kununua mkataba wake

Zamunda alisema anataka kupata chochote katika mauzo ya mchezaji huyo kutokana na kwenye kipengele chake cha mkataba inasema kuna asilimia anatakiwa apate.

“Omary anatakiwa alipe hela kwani hana timu inayomtaka, Awadh klabu inayomhitaji inabidi iniandikie barua na kama ikiwezekana nipate asilimia 20 atakapouzwa,” alisema Zamunda.

Advertisement