Mkuu wa Mkoa Mtwara avunja uongozi Ndanda FC

Muktasari:

Timu ya Ndanda FC ya mkoani Mtwara iliyokwama mkoani Singida kutokana na ukata tayari imeondoka mkoani humo kurejea nyumbani kwa ajili ya kuweka kambi kujiandaa na mechi zinazofuata.

Mtwara. Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa ameuvunja uongozi wa Ndanda FC na kuunda kamati ya muda ya wajumbe kumi itakayosimamia timu hiyo kwa kipindi cha msimu wa Ligi Kuu uliosalia bila kuathiri katiba ya timu hiyo.

Byakanwa ambaye ni Mlezi wa Ndanda ameyasema hayo leo Ijumaa, Oktoba 12, kamati hiyo itaongozwa na mwenyekiti, Laurent Werema itasimamia maslahi kutokana na uongozi uliopo kuonekana kuelemewa hali iliyosababisha hivi karibuni timu hiyo kukwama mkoani Singida.

Amesema timu hiyo inachangamoto za kifedha ambazo ziko katika kila timu na kufafanua kwamba klabu hiyo imecheza mechi nyingi ugenini na hivyo kukosa mapato (gate collection) na kwamba uamuzi wa kuiundia kamati ni kuinusuru.

“Kama mlezi wa timu nakiri hali ngumu ya uchumi ndani ya klabu, lakini bado tunafanya jitihada za kuhakikisha timu naondoka katika hiyo hali na inaweza kushiriki mechi nyingine, mpaka sasa timu iko njiani kuja Mtwara kuingia kambiini kwa ajili ya maandlizi ya mechi zinazofuata,”amesema Byakanwa

“Kama mlezi hatuwezi kuendelea kuingalia timu ikiwa katika hayo mazingira isipokuwa tunahitaji kufanya uamuzi yanayoweza kuisaidia timu kuendelea kufanya vizuri... tumekaa na viongozi wetu tumeona msalaba wanaoubeba wale viongozi na tumeamua kufanya uamuzi wa kuweka uongozi pembeni na kuunda kamati itakayosimamia kwa msimu wote,”amesema

Amefafanua kwamba hawajavunja katiba ya Ndanda, kuondoa viongozi wa Ndanda madarakani isipokuwa wamewekwa pembeni na kuundiwa kamati itakayosimamia timu kwa maslahi ya timu na kuendelea vizuri hadi msimu utakapokwisha na kufanywa tathimini.

Mkazi wa Mtwara, Hassan Jumbe amepongeza hatua hiyo na kusema italeta ufanisi zaidi katika klabu hiyo.

“Kuundwa kwa kamati ni jambo jema kwa sababu kama inafikia wakati timu inakwama ugenini kutokana na kukosa fedha ni kitendo ambacho kitawaathiri wachezaji hivyo ni wazo nzuri kama kamat hiyo itakwenda kusimamia yale yaliyokusudiwa ili timu yetu iendelee kubaki ligi kuu,” amesema Jumbe

Hata hivyo mkuu wa mkoa amemshukuru msanii wa bongo fleva Harmonize kwa kuchangia klabu hiyo Sh 3.4 milioni na kumuomba kuridhia kuwa mmoja wa wanakamati hiyo.