Mkhitaryan ruksa kuwavaa Chelsea

Muktasari:

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Azerbaijan, Leyla Abdullayeva alisema mambo ya kisiasa hayawezi kupewa nafasi na kuwa kikwazo cha kumzuia mchezaji huyo asiende kuisaidia timu yake kubeba ubingwa.

STAA wa Arsenal, Henrikh Mkhitaryan ameambiwa na maofisa wa Azerbaijan kwamba ataruhusiwa kuingia kwenye nchi hiyo kwenda kuitumikia timu yake katika fainali ya Europa League dhidi ya Chelsea, Mei 29.
Kulikuwa na wasiwasi wa kiungo huyo kushindwa kwenda kucheza katika fainali hiyo itakayofanyika kwenye mji wa Baku baada ya kuwapo na tofauti za kisiasa baina ya nchi yake ya Armenia na Azerbaijan, ambazo ziliwahi kupigana vita miaka mitatu iliyopita.
Hofu ya awali ilikuwa kwamba huenda Mkhitaryan asingeruhusiwa kupata kibali cha kuingia nchi hiyo baada ya uhasama huo ambao haukupatiwa ufumbuzi wowote wa kidiplomasia.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Azerbaijan, Leyla Abdullayeva alisema mambo ya kisiasa hayawezi kupewa nafasi na kuwa kikwazo cha kumzuia mchezaji huyo asiende kuisaidia timu yake kubeba ubingwa.
Alisema: "Matukio makubwa sana ya michezo yamefanyika Azerbaijan na wanamichezo wa Armenia wamekuja kushiriki. Michezo na siasa ni vitu viwili tofauti."
Hata hivyo, Arsenal bado wanataka kuhakikishia na Uefa kuhusu usalama wa mchezaji wao atakapokwenda Baku. Arsenal inahitaji kushinda Europa League ili kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.