Mkenya awaganda Bocco na Kagere tu

Tuesday September 11 2018

 

By CHARITY JAMES NA OLIPA ASSA

KOCHA wa AFC Leopard, Thomas Juma ameshindwa kujizuia na kufichua namna anavyowatazama kiufundi nyota wa Simba, John Bocco na Meddie Kagere kuona mmoja wapo anaweza akabeba kiatu cha dhahabu cha Ligi Kuu Bara.

Alianza kwa kumwelezea Bocco na kukiri alikuwa mwiba kwa mabeki wake, wakati wa mechi yao ya kirafiki ambayo Simba ilishinda mabao 4-2, huku Bocco akitupia kambani mawili, na mengine yakifungwa na Mohammed Ibrahim na Marcel Kaheza.

“Simba ina wachezaji wengi wazuri, aliyenikosha ni nahodha wao (Bocco), kwanza ana nidhamu ya hali ya juu, anajituma, kwa kifupi ana kila kitu, akiendelea hivyo katika ligi yao anaweza akawa mfungaji wa ligi,” alisema.

Mbali na Bocco alimtaja Kagere na kutamani angekuwepo katika mchezo huo kwa madai vitu anavyovifanya Ligi Kuu Bara, vinapenya mpaka anga la Kenya na kudai mbio za ufungaji zitawahusu zaidi wao msimu huu.

Kocha huyo alisema walitamani kuona Kagere atafanya kitu gani katika mechi hiyo, hasa baada ya kutoka na moto Gor Mahia kuja kujiunga na Simba.

“Nimesikitika sana kumkosa Kagere katika mechi hii, nilitamani kumfuatilia kila hatua kwa dakika ambazo angecheza, bado ana madini mengi na kama si nahodha wao kuchukua kiatu basi atakuwa yeye,” alisema.

Licha ya kudatishwa na mastaa hao, pia aliielezea Simba endapo kama Kocha Patrick Aussems hatakuwa makini kurekebisha safu ya ulinzi basi atakuwa anafanya kazi ya bure.

“Simba ina udhaifu kwenye beki, ndio maana hata katika mchezo wetu tuliwafunga dakika za mwishoni, washambuliaji wanafanya kazi kubwa, ila wanaangushwa na mabeki, hawapo makini katika kazi yao,” alisema.

Kocha huyo alisema japo hajaziona timu nyingine za Tanzania zikicheza, ila anaamini kama Simba itarekebisha tatizo hilo la mabeki itaweza kutisha na kutetea taji lao.

Advertisement