Mkenya aanika siri nzito VPL

KOCHA wa Biashara United, Francis Baraza amefichua kitu kinachowaangusha wachezaji wengi wa Tanzania wenye vipaji kushindwa kufika mbali, amegundua wameshindwa kuthamini kazi zao na kujua jinsi wanavyochukuliwa katika jamii.

Baraza amesema tangu aanze kuifundisha Biashara, ameona vipaji vikubwa, lakini kinachomshangaza ni aina ya maisha ya wachezaji hao wanavyochukulia kazi zao na jinsi ambavyo wanajiweka kuwa wa kawaida wakati soka ndilo linalopendwa zaidi duniani.

Kocha huyo ameshauri kuwa wachezaji wanapaswa kujengwa kisaikolojia ili wanapofanya kazi wajue uzito wa namna mchezo wenyewe unavyochukuliwa kwenye jamii, akisisitiza kwamba likifanyika hilo anaona wengi maisha yao yatabadilika.

“Asilimia kubwa wengi wana uwezo mkubwa, ukiwaangalia unawaona mbali, lakini matendo yao yanakinzana na miguu yao, sasa basi hata wale wanaowazunguka wakiwaambia ukweli soka linataka nini kuliko kuwadanganya, naamini mabadiliko yatakuja kutokea mpaka kwenye timu ya Taifa,” amesema.

Baraza ametoa mfano wa Mbwana Samatta anayecheza Fenerbahçe ya Uturuki kwa mkopo akitokea Aston Villa ya Ligi Kuu ya England, anaamini ana watu sahihi wanaomjenga kiakili na kujitambua kwamba yeye ni nani mbele ya watu wanaofuatilia soka duniani. “Nina asilimia kubwa kwamba wachezaji wengi wanayatamani maisha ya Samatta ambaye ni Mtanzania mwenzao, sasa kama imewezekana kwa huyo, wao wajiulize njia zao ni zipi, ingawa kila mtu anaweza akawa na fungu lake,” amesema.

Naye Kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alikazia pointi aliyozungumza Baraza kwamba, wachezaji wazawa wakijitambua hata thamani yao ya malipo itakuwa kubwa kama ilivyo kwa mastaa wa kigeni.

“Ndio maana tunawaona mastaa wa kigeni wana viwango, siku zote nimekuwa nikisema wanafanya kazi kulingana na kile wanachokipata, pia wanalinda kile wanachokipata ili wapate zaidi, hilo lingekuwa chachu kwao kutokukubali hilo.”