Mke wa Suarez apiga kijembe Barca

MADRID HISPANIA. MKE wa straika,Luis Suarez mrembo Sofia Balbi ni kama anawacheka Barcelona baada ya mumewe kuanza kwa gia kubwa kwenye klabu yake mpya ya Atletico Madrid.

Straika, Suarez aliwaonyesha Barcelona kila watakachokikosa baada ya kufunga mara mbili na kuasisti mara moja kwenye mchezo wake wa kwanza akiwa na Atletico Madrid na alikuwa uwanjani kwa dakika 19 tu kuisaidia timu hiyo kushinda 6-1 dhidi ya Granada kwenye mchezo wa La Liga.

Mrembo Sofia hakutaka kuchelewesha mambo kwa kuwatupia kijembe mabosi wa huko Nou Camp, wakati alipoandika kwenye mtandao wa kijamii: “Hiki ndicho mnachostahili!”

“Raha kiasi gani kuwaona mkijicheka wenyewe.”

Hata mke wa Lionel Messi, mrembo Antonella Roccuzzo, alijibu ujumbe huo wa rafiki yake kwa kuweka emoji nyingi tu za kupiga makofi.

Mrembo Antonella alimtoa machozi rafiki yake Sofia kwa ujumbe mzito wa kuagana naye wakati wanafamilia hao marafiki walipoondoka Barcelona na kuhamia Madrid.

Straika huyo wa zamani wa Liverpool, Suarez alitua Atletico kwa Pauni 5.5 milioni baada ya kocha mpya wa huko Nou Camp, Mdachi Ronald Koeman kumwambia hana tena mpango wa kuendelea kumtumia kwenye kikosi chake.

Licha ya kubeba mataji tisa akiwa na Barcelona, Suarez alionekana si kitu na kufunguliwa mlango wa kutokea huku akiwa mchezaji namba tatu wa muda wote kwenye kufunga mabao na amefunga mara 198 katika mechi 283 alizotumikia miamba hiyo.

Mastaa kibao wa zamani wa Barcelona, akiwamo Neymar na Samuel Eto’o hawakupendezwa na namna Suarez alivyoachwa.