Mke wa Reyes afichua meseji kabla mumewe kufa

Muktasari:

Reyes, 35, na binamu yake Jonathan Reyes, 23, wote walifariki dunia kwenye ajali hiyo ilitokea kwenye Mji wa Alcala de Guadaira Kusini mwa Hispania.

SEVILLE, HISPANIA. MJANE wa staa wa zamani wa Arsenal, Jose Antonio Reyes mrembo, Noelia Lopez ametuma meseji ya mwisho kabisa aliyotumiwa na mumewe kwenye WhatsApp saa kadhaa kabla ya winga huyo kupoteza maisha katika ajali mbaya ya gari.

Staa huyo wa zamani wa kimataifa wa Hispania, Reyes aliripotiwa kutuma mesaji iliyosomeka hivi “Habari za asubuhi mami, nawapenda,” kwa mkewe kupitia WhatsApp ikiwa ni salamu kwa familia yake aliyokua ameiacha nyumbani. Meseji hiyo iliingia kwenye simu ya mrembo Noelia saa nne kabla ya ajali mbaya, ambapo mama huyo wa watoto wa Reyes alikuwa amemsevu mume wake kwenye simu yake kwa jina la ‘Daddy Love’.

Reyes, 35, na binamu yake Jonathan Reyes, 23, wote walifariki dunia kwenye ajali hiyo ilitokea kwenye Mji wa Alcala de Guadaira Kusini mwa Hispania.

Binamu mwingine wa Reyes, Juan Manuel Calderon, 22, aliungua vibaya sana wakati alipokuwa akijaribu kuwaokoa wenzake kutoka kwenye gari wakati moto ulipokuwa unawaka.

Ripoti zinadai Reyes alikuwa kwenye mwendo kasi sana kabla ya ajali hiyo kutokea.

Reyes alikuwa Mhispaniola wa kwanza kushinda taji la Ligi Kuu England akiwa na Arsenal. Alibeba pia ubingwa wa La Liga akiwa na Real Madrid na alinyakua mataji matatu ya Europa League akiwa na kikosi cha Sevilla.