Mkamba yapokwa pointi SDL

Muktasari:

Kanuni zilizopitishwa na shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) inazitaka timu mwenyeji katika ligi wanazosimamia kuandaa gari la wagonjwa, vijana wa kuokota mipira na watu wa huduma ya kwanza (Red Cross) na mojawapo likikosekana timu mwenyeji hupokonywa alama tatu.

Timu ya soka ya Mkamba Rangers imepokonywa alama tatu na mabao mawili na kupewa Dar City Fc ligi daraja la pili Tanzania bara (SDL) 2019/2020 baada ya mchezo wao kuchezwa kwa dakika tatu pekee katika uwanja wa jamhuri mkoani Morogoro.
Mchezo huo ulisimamishwa na mwamuzi, Coleman Mushi baada ya Mkamba Rangers Fc kushindwa kutimiza baadhi za kanuni za ligi daraja la pili kwa timu mwenyeji kuandaa gari la wagonjwa.
Kanuni zilizopitishwa na shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) inazitaka timu mwenyeji katika ligi wanazosimamia kuandaa gari la wagonjwa, vijana wa kuokota mipira na watu wa huduma ya kwanza (Red Cross) na mojawapo likikosekana timu mwenyeji hupokonywa alama tatu.
Mwamuzi ya mwamuzi wa kati, Coleman Mushi, Kamisaa wa mchezo huo, Pascal Bela na wasaidizi wa pembeni, Ibrahim Hasian na Wema Kapinga pamoja na mwamuzi wa akiba, Sebastian Sanga walikubaliana mchezo huo kusimamishwa mpaka gari la wagonjwa liwepo uwanjani.
Akizungumza na gazeti hili uwanjani hapo mkoani hapa, Kocha mkuu wa timu ya Dar City Fc, Almasi Shabaan alisema kuwa wamefurahishwa kupata alama tatu na mabao mawili baada ya wenyeji wao Mkamba Rangers Fc kushindwa kutimiza moja ya kanuni inayomtaka mwenyeji kuandaa gari la wagonjwa  uwanjani.
Almasi alisema kuwa kupata alama hizo imekuwa faida kwa timu yao ambayo imepoteza michezo miwili na kupata sare mchezo mmoja kabla ya kupata alama tatu za bure kutoka kwa Mkamba Rangers Fc katika mchezo wao wa nne katika ligi hiyo.
“Ukidharau kanuni za TFF zinazotaka timu mwenyeji kuandaa gari ya wagonjwa, watu wa huduma ya kwanza na vijana wa kuokota mipira, mwamuzi atasimamisha mchezo kwa dakika 15 na isipotekelezwa atamaliza mchezo na wapinzani wao kupewa alama tatu na mabao mawili ndio tulivyofaidika Dar City Fc.”alisema Almasi.
Kwa upande wa meneja wa Mkamba Rangers Fc, Kelven John Nashi alisema kuwa kukosekana kwa gari la wagonjwa uwanjani hapo imetokea kutokubaliana na watu wa huduma ya kwanza katika kikao chao na maafisa wa chama cha soka mkoa wa Morogoro kabla ya mchezo huo.
“Sisi kama Mkamba Rangers Fc tuliomba tuchangie gharama za sh40,000 kwa ajili ya gari ya wagonjwa na fedha tulikuwa tayari kutoa baada ya mchezo lakini hatukuweza kueleweka mpaka hali hii imejitokeza kwa mchezo kusimama dakika tatu baada ya kuanza kuchezwa.”alisema Kelvin.
Kelvin alisema Sintofahamu hiyo kwao ni hasara kwani kupoteza alama tatu imewarudisha nyuma na morali katika harakati za kuwania nafasi ya kwanza katika kundi lao.
“Tumecheza michezo nne na kupoteza michezo mitatu tukishindamchezo mmoja dhidi ya Mpwapwa United kwa bao 2-1, leo (jana) tukipiga hesabu za kupata matokeo mbele ya Dar City Fc yanatokea hayo.”alisema Kelvin.
Kelvin alisema kuwa timu ya Mkamba Rangers Fc ipo katika mazingira mangumu kwa mdau, Batazali Mtitu kuisaidia timu kwa kutoa fedha za kuisafirisha kwa michezo ya nje ya kijiji cha Mkamba wilaya ya Kilombero baada ya uwanja wao kufungiwa na TFF kwa kukosa sifa.