Mkali wa mabao Afcon afariki dunia

Muktasari:

Taji hilo la 1974 lilikuwa la pili la mwisho kwa DR Congo lilimpa heshima kubwa straika huyo ambaye kwa mujibu wa Waziri wa Michezo wa nchi hiyo, Papy Niango, marehemu alikuwa Afrika Kusini akipata matibabu tangu Agosti mwaka jana

STRAIKA wa zamani wa DR Congo anayeshikilia rekodi ya Mfungaji Bora katika Fainali za michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), Pierre Ndaye Mulamba amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 70.
Mkali huyo aliyeandikisha rekodi ya kufunga mabao tisa katika fainali za mwaka 1974 zilizofanyika nchini Misri, inaelezwa alikumbwa na mauti hayo mwishoni mwa wiki mjini Johannesburg, Afrika Kusini.
Rekodi hiyo ya Mkongoman huyo aliyeichezea timu ya taifa ya nchi yake tangu mwaka 1967 hadi 1978 anakumbukwa kwa kuipa nchi yake taji katika michuano hiyo wakati walipoifunga Zambia kwenye fainali kali. Mabao yake 9 yaliyompa tuzo ya Mfungaji Bora hayajawahi kuvunjwa tena na straika yeyote katika michuano hiyo ya Afrika.
Taji hilo la 1974 lilikuwa la pili la mwisho kwa DR Congo lilimpa heshima kubwa straika huyo ambaye kwa mujibu wa Waziri wa Michezo wa nchi hiyo, Papy Niango, marehemu alikuwa Afrika Kusini akipata matibabu tangu Agosti mwaka jana.
Kabla ya kwenda Afrika Kusini alipokuwa akiishi kama Mkimbizi, alikuwa akienda mara kwa mara kupatra matibabu nchini India akisumbuliwa na tatizo la figo na ugonjwa wa moyo mbali na tatizo la goti lililotokana na kushambuliwa kwa risasi na majambazi mwaka 1994.
Gwiji huyo aliyefahamika kisoka kama Mutumbula anakumbukwa kwa jinsi alivyowahi kuisaidia pia klabu yake ya AS Vita aliyokuwa anaichezea kubeba taji la Afrika mwaka 1973.
Katika fainali za mwaka 1974, alifunga mara mbili dhidi ya Guinea na jingine moja walipovaana na Mauritius katika makundi  na kufunga mengine kwenye mechi za nusu fainali dhidi ya waliokuwa watetezi Misri na Zambia kwenye fainali na kuibebesha timu yake taji hilo.
Rekodi ya ufungaji mabao kwa ujumla katika Afcon inashikiliwa na Mcameroon Samuel Eto'o, aliyefunga mabao 18.