Mkali Divock Origi atulizwa huko Anfield

Thursday July 11 2019

 

LIVERPOOL, ENGLAND. Shujaa wa Liverpool kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Divock Origi ametulizwa huko Anfield baada ya kupewa dili la mkataba mrefu wa kuendelea kukitumikia kikosi hicho kinachonolewa na Mjerumani.

Staa huko Mbelgiji mwenye asili ya Kenya, ambaye alifunga kwenye mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Tottenham Hotspur mwezi uliopita, amesaini mkataba mpya wa kudumu Anfield juzi Jumatano.

Straika huyo mwenye umri wa miaka 24 alisema kwamba siku zote alikuwa na matarajio ya kubaki Merseyside, akisema: "Ndiyo, nina furaha kwa kusaini mkataba huu kwa sababu unanipa hamasa ya kuanza vyema msimu mpya kama ulivyomalizika uliopita.

"Nimepiga hatua katika maisha yangu ya mpira, Ninachoweza kusema nimekuwa mwanamume katika klabu hii, ambayo mara ya kwanza nilisaini nikiwa na umri wa miaka 19."

Origi amekuwa kwenye kikosi cha Liverpool tangu aliponaswa kutoka Lille kwa ada ya Pauni 10 milioni mwaka 2014. Baada ya mkataba wake wa miaka mitano kufika mwisho, mashabiki walihitaji mshambuliaji huyo abaki kutokana na ushujaa wake aliofanya msimu uliopita.

Origi alifunga mara mbili wakati walipowatupa nje Barcelona kisha alikwenda kufunga kwenye mchezo wa fainali dhidi ya Spurs huko Wanda Metropolitano.

Kocha Jurgen Klopp alisema anadhani usajili wa mchezjai huyo ni ushindi wa pande zote mbili, klabu na mchezaji. Origi alicheza mechi 21 msimu uliopita na kufunga mabao saba.

Advertisement