Mitambo ya mabao Ligi Kuu England msimu huu

Monday January 14 2019

 

LONDON, ENGLAND.LIGI Kuu England utamu umezidi kunoga kutokana na mchakamchaka wake kufikia patamu kwelikweli. Vita ni kali kwa sasa katika kila idara, kwenye mbio za ubingwa, Top Four na hata kwenye mchakamchaka wa kufukuzia Kiatu cha Dhahabu.

Hakuna mchezaji anayetaka kuachwa mbali huko kwenye vita ya kuanzia Kiatu cha Dhahabu kutokana na sasa kuwapo kwa wachezaji watatu waliokabana koo kwa kufunga mabao 14 kila mmoja.

Lakini, ligi hiyo imeshuhudia wachezaji wengi waliohusika kwenye mabao mengi na hawa ndio baadhi yao walihusika kwenye mabao yanayoanzia tarakimu mbili.

Mohamed Salah - mabao 21, dakika 1,848

Supastaa wa Liverpool, Mohamed Salah ameendelea kuwa mtu muhimu kabisa kwenye kikosi hicho cha Anfield baada ya kuhusika kwenye mabao 21 katika dakika 1,848 alizocheza kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Mo Salah amefunga mabao 14 na kuasisti saba kwenye dakika hizo, huku akipiga jumla ya mashuti 55 na 36 yakilenga goli la wapinzani.

Eden Hazard - mabao 20,dakika 1,672

Fundi wa mpira wa Chelsea, Eden Hazard ameingia kwenye rekodi za kufunga na kuasisti kwa mabao yanayoanzia tarakimu mbili huko kwenye Ligi Kuu England baada ya kuhusika kwenye mabao 20 katika dakika 1,672 alizoitumikia Chelsea kwenye ligi hiyo. Hazard amefunga mabao 10 na kuasisti mengine 10, huku akiwa amepiga mashuti 32 tu na 25 yakiwa ndio yaliyolenga golini kwa wapinzani.

Harry Kane - mabao 18,dakika 1,707

Straika matata kabisa wa Tottenham Hotspur, Harry Kane amehusika kwenye mabao 18 kwenye Ligi Kuu England kabla ya mchezo wa jana Jumapili alipowakabili Manchester United uwanjani Wembley. Fowadi huyo amefunga mabao 14 na kuasisti mengine manne kwenye dakika 1,797 alizoitumikia Spurs kwenye Ligi Kuu England msimu huu huku akipiga mashuti 54 na 33 kati yake ndio yaliyolenga goli.

Aubameyang - mabao 17,dakika 1,737

Staa wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang ni miongoni mwa wachezaji waliohusika kwenye mabao mengi kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Aubameyang kwenye ligi hiyo msimu huu amecheza dakika 1,737 na kuhusika kwenye mabao 17, akifunga 14 na kuasisti matatu. Kwenye dakika hizo alizocheza, Aubameyang amepiga mashuti 45 huku 24 yakiwa yamelenga golini.

Raheem Sterling - mabao 16, dakika 1,479

Kocha Pep Guardiola baadhi ya wachezaji wake anaojivunia kuwa nao kwenye kikosi cha Manchester City mmoja wao ni Mwingereza Raheem Sterling. Hakika staa huyo amefanya vyema kwenye ligi hiyo msimu huu akihusika kwenye mabao 16, akifunga tisa na kuasisti mengine saba katika dakika 1,479 alizocheza huku akipiga pia mashuti 25 na 19 yakilenga kwenye magoli ya wapinzani.

Sergio Aguero - mabao 15,dakika 1,258

Straika wa Manchester City, Sergio Aguero hakika ni mmoja wa wachezaji ambao suala la mabao kwenye Ligi Kuu England halijawahi kuwa shida kwao. Kwenye ligi hiyo msimu huu, Aguero amehusika kwenye mabao 15 baada ya kucheza dakika 1,258. Kwenye mabao hayo, Aguero amefunga mara 10 na kuasisti mara tano, huku akipiga mashuti 49 kwa ujumla wake huku 23 yakilenga golini.

Callum Wilson - mabao 14,dakika 1,658

Straika wa Bournemouth, Callum Wilson ni mmoja wa wachezaji wanaofanya vyema kabisa kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Fowadi huyo kiwango chake kimemfanya aanze kufukuziwa na Chelsea kwenye dirisha hili la Januari hasa baada ya kuhusika kwenye mabao 14 katika dakika 1,658 alizocheza kwenye ligi hiyo. Wilson amefunga mabao tisa na kuasisti matano huku akipiga mashuti 34 na mashuti yake 18 yakiwa pekee yaliyolenga kwenye magoli ya wapinzani.

Paul Pogba - mabao 13,dakika 1,496

Kiungo wa Manchester United, Paul Pogba jana Jumapili alitarajia kuwamo uwanjani kwenye mchezo mkali dhidi ya Tottenham Hotspur huko Wembley. Rekodi zake kwenye Ligi Kuu England kabla ya mechi hiyo, Pogba amehusika kwenye mabao 13, akifunga saba na kuasisti mara sita. Staa huyo pia amepiga mashuti 44 na 31 yakiwa yamelenga kwenye magoli ya wapinzani. Staa mwingine aliyehusika kwenye mabao 13 ni fowadi wa Tottenham Hotspur, Son Heung-Min, ambaye amefunga manane na kuasisti mara tano kwenye dakika 996 alizocheza, akipiga mashuti 30 na 17 ndiyo yaliyolenga goli.

Alexandre Lacazette - mabao 12, dakika 1,380

Straika wa Arsenal, Alexandre Lacazette ni mmoja wa wachezaji tishio kwenye Ligi Kuu England msimu huu kutokana na mchango wake anaotoa kwenye kikosi hicho cha Emirates. Fowadi huyo wa kocha, Unai Emery amehusika kwenye mabao 12, akifunga mara saba na kuasisti matano katika dakika 1,380 alizocheza kwenye michuano hiyo. Amepiga mashuti 34 huku 17 tu ndio yaliyolenga goli.

Roberto Firmino - mabao 11, dakika 1,701

Fowadi wa Liverpool, Mbrazili Roberto Firmino ni miongoni mwa mastaa wa maana ambao wamekuwa wakihusika kwenye mabao mengi huko kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Fowadi huyo amehusika kwenye mabao 11, akifunga mara nane na kuasisti matatu katika dakika 1,701 alizocheza huku akipiga mashuti 38 na 23 yakilenga goli.

Mchezaji mwingine aliyehusika kwenye mabao 11 ni kiungo wa Everton, Gylfi Sigurdsson, aliyefunga mara nane na kuasisti mara tatu kwenye dakika 1,710 alicheza, akipiga mashuti 33 na 18 yakilenga goli.

Advertisement