Mitambo imewaka...

Thursday August 9 2018

 

By WAANDISHI WETU

ACHANA na matokeo ya jana Jumatano pale Uwanja wa Taifa, ukweli ni kwamba mitambo ya Simba imewaka, hii ni baada ya Wekundu wa Msimbazi hao, kuonyesha soka tamu hasa Mzambia, Cletus Chama, aliyeupiga mwingi na kuwazima Waghana wa Asante Kotoko.

Simba ilihitimisha Wiki ya Tamasha la Simba Day kwa kulazimisha sare ya bao 1-1 huku ikishuhudiwa Adam Salamba akiiinyima timu yake ushindi baada ya kupiga penalti nyepesi dakika za jioni.

Tamasha hilo la Simba lililohudhuriwa na zaidi ya mashabiki 50,000 lilipambwa na burudani kemkem za muziki toka kwa wasanii kama Tundaman, Chid Benz na Msaga Sumu sambamba na bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’.

Katika mchezo huo, Kotoko iliyochezesha asilimia kubwa ya wachezaji vijana, ilionyesha soka tamu na kuwapa kipimo kizuri wenyeji wao ambao hii ni mechi yao ya kwanza jijini Dar es Salaam tangu iwe chini ya Kocha, Patrick Aussems.

MCHEZO ULIVYOKUWA

Tangu kipindi cha kwanza kilipoanza, Simba ilianza kwa kazi na kushambulia lango la Kotoko, lakini umakini wa ukuta wa timu hiyo ikibebwa na umahiri wa kipa Felix Hanan ambaye aliokoa michomo mingi ya wazi ya nyota wa Simba Emmanuel Okwi na Meddie Kagere walioshirikiana vyema kabla ya Kagere kupumzishwa.

Dakika 14 tu ya mchezo huo beki Shomary Kapombe aliumia baada ya kugongana na beki wa Kotoko na kutolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Nicholas Gyan, kutolewa kwa beki huyo kuliwapa nafasi wageni kuliandama lango la Simba.

Sekunde chache kabla ya mapumziko, Kotoko iliwanyamazisha mashabiki wa Simba baada ya Michael Yeboah kufunga bao kwa kichwa akimalizia mpira wa shuti uliogonga besela na kurudi na Yeboah kumzidi ujanja Pascal Wawa.

Licha ya bao hilo, lakini ukweli ni kwamba Simba ilitawala sehemu kubwa ya mchezo huo huku Mzambia Chama akifunika kwa soka lake tamu akishirikiana na Jonas Mkude na James Kotei katika eneo la kati.

Katika kipindi cha pili, Kocha Aussems alimtoa Kotei na kumwingiza Hassan Dilunga na baadaye kumtoa Kagere na aliyempisha Adam Salamba na kuifanya Simba irudi mchezoni kwa kasi na kuliandamana lango la wapinzani wao.

OKWI KAMA KAWA

Licha ya Okwi kukosa mabao mengi ya wazi kiasi cha baadhi ya mashabiki kutamani kuona anatolewa, Mganda huyo kama kawaida aliendelea kuwapa raha Simba kwa kuiokoa na kipigo kwa kufunga bao la kusawazisha katika dakika ya 76.

Bao hilo lilifungwa na Okwi kwenye eneo gumu, akiwahi krosi pasi ya Shiza Kichuya, aliyewasumbua mabeki wa Kotoko ambao ilikuwa ni mara yao ya kwanza kuja kucheza na Simba jijini Dar es Salaam.

Dakika ya 85, Salamba alichezewa madhambi na kumfanya mwamuzi, Hans Mabena kuamuru penalti iliyolalamikiwa na wachezaji wa Kotoko, lakini straika huyo mpya aliyetua akitokea Lipuli ya Iringa, alishindwa kuukwamisha wavuni baada ya mkwaju wake kudakwa na kipa Hanan.

WAZIRI LUGOLA WAMO

Kama kawaida Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, ambaye tangu ateuliwa kushika nafasi hiyo kumrithi, Mwigulu Nchemba aliendelea kutema cheche zake kwa kuwatangazia kiama wapiga fedha wanaouza jezi feki za klabu.

Lugola aliyemwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alitema cheche hizo muda mchache baada ya kukagua timu hizo na kusema kuanzia sasa wauza jezi feki za klabu iwe za Simba, Yanga ama timu nyingine wakatafute cha kufanya kwani serikali itawasaka kila kona kwa nia ya kuziwezesha klabu kunufaisha na rasilimali zao.

CHAMA NOMA SANA

Kama kuna mchezaji aliyekuna nyoyo za mashabiki kwa soka lake la kuvutia, basi ni Mzambia Chama aliyelifanya soka lionekane kama mchezo mwepesi kwa jinsi alivyokuwa akiumiliki na kugawa ‘vyumba’ kwa nyota wenzake.

Chama aliyesajiliwa Msimbazi akitokea Lusaka Dynamos, alionyesha ni kiungo anayejua majukumu yake, licha ya ugeni wake ndani ya kikosi hicho na kuwafanya mashabiki kumshangilia kila alipogusa mpira katika mchezo wa jana.

CHAZ BABA, KALALA JR WATEKWA

Pesa noma sana, waimbaji wa Twanga Pepeta, Kalala Junior na Charles Baba ambao wanafahamika ni mashabiki wa Yanga, jana walilazimika kuishabiki Simba bila kupenda.

Wakiwa wamevalia jezi za sare ya Simba huku nyuma zikiwa na majina yao, walishindwa kutofautishwa na manazi wa Msimbazi na kushindwa kufuata nyayo za Sunday Manara, nyota wa zamani wa Yanga alimgomea mwanaye, Haji Manara, aliyetaka kumvisha jezi ya Simba.

Manara alimtambulisha baba yake sambamba na nyota wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni kisha kumtaka avae uzi wa Msimbazi na nyota huyo wa zamani wa Yanga, Pan African na Taifa Stars akachomoa.

Hata hivyo kwa Chaz Baba na Kalala Jr, walishindwa na walifichua kilichowafanya kuvaa uzi wa Msimbazi kwa kusema

“Ebwana mpango wa pesa dada si unajua. Jana tu ndio tulichukua maamuzi haya,”alisema Chaz Baba.

Waimbaji hao maarufu katika miondoko ya bolingo, waliambatana na bendi ya Twanga Pepeta na kutumbuiza katika sherehe hizo.

SIMBA

Manula, Kapombe/Gyan, Kwasi, Nyoni, Wawa, Mkude, Chama, Kotei/Dilunga, Kagere/Salamba, Okwi na Kichuya.

Imeandikwa na Thobias Sebastian, Charles Abel na Doris Maliyaga

Advertisement