Miss Simba: UD Songo noma cheki ilichomfanya

KAMA ulizoea kuiona sura ya shabiki kindakindaki wa Yanga, Ally Yanga (sasa marehemu) pekee akiwa kivutio viwanjani enzi zake, basi na pale Msimbazi yuko huyu mwanadada mrembo ambaye ni Simba lialia, Agnes Malkia Daniel.

Akienda kwa jina utani la Miss Simba, mwanadada huyu ni shabiki wa kutupwa wa mabingwa hao mara mbili mfululizo wa Ligi Kuu ya Bara ambao wanajiandaa kutwaa taji lao la tatu mfululizo ligi itakaporejea baada ya mapumziko ya janga la corona.

Kuna mashabiki wengi wa kike wa timu za soka nchini. Ndio hapo unaweza kujiuliza kwanini Miss Simba?

Huyu dada buana amefanya jambo tofauti katika kuthibitisha mapenzi yake kwa Wekundu wa Msimbazi.

Amekubali kuingia gharama na kupitia maumivu makali ya sindano za moto na kujiweka alama zisizofutika kirahisi mwilini kwa kuchorwa tattoo kadhaa za kuinadi Simba.

Bega moja amechorwa tattoo kubwa ya kichwa cha mnyama simba, bega jingine ameweka tattoo ya nembo ya klabu ya Simba na mkononi ameandika neno refu: “Miss Simba Sport Club’.

Utamaduni wa kuchorwa tattoo umeanza kuwa maarufu nchini lakini kwa mwanamke kuchorwa tattoo za klabu ya mpira wa miguu si jambo jepesi sana.

Mwanaspoti imepiga stori na mwanadada huyu ambaye huwa hakosekani kwenye shughuli za uhamasishaji za timu hiyo hasa kwenye Jukwaa Kuu viwanjani na kwenye mitandao ya kijamii.

ALIANZA VIPI KUIPENDA SIMBA

“Nilijikuta naipenda Simba kutokana na wazazi wangu kuwa mashabiki wa mpira. Baba yangu ni Simba na mama yangu ni Yanga, mimi nikamfuata baba, si unajua watoto wa kike na baba zetu, basi nikiwa mdogo sijitambui naipenda, sasa najitambua nikaona nionyeshe kweli mahaba yangu.

“Nimehamasika kutokana na familia yangu kuwa familia yenye ushabiki wa mpira, pia kutokana na kwamba soka ndo burudani ninayoipenda kuliko burudani nyingine zote’’

MWITIKIO WA

WANAWAKE

‘’Nafikiri nitakuwa nimewavutia wanawake wengi sana siyo tu kwenye mitandao ya kijamii, nafikiri hata katika mazingira ninayoishi, maana nimeona watu wanavyohamasika na kuipenda Simba na soka kwa ujumla.”

Agnes anasema, anatamani kuona wanawake wanazidi kuwa wengi katika kushabikia timu, kwa kuwa mpira ni starehe nzuri na pia inajenga umoja na kuongeza idadi ya marafiki kuliko maadui.

SIMBA INAPOFUNGWA

“Kama mwanachama na shabiki lazima naumia sana hasa kwa kitu unachokipenda lazima itakuuma sana mwisho wa siku unajua mpira wa miguu uko na matokeo ya kikatili sana wakati mwingine kwa kuwa mimi ni mpenzi wa mpira na natambua hakuna timu isiyofungwa so maisha lazima yaendelee,”

MUME/ BOIFRENDI?

“Mie huwa napenda kuangalia kitu moyo wangu unapenda kufanya ili mradi sivunji sheria, mwanaume inabidi anikubali nilivyo na aheshimu kile ninachokipenda, japokuwa sipendi sana kuzungumzia maisha yangu binafsi.”

TATTOO ZA SIMBA

Mwanadada huyu kulingana na mahaba yake na Wekundu hao wa Msimbazi aliamua kuchora tattoo zinazoonyesha nembo ya klabu hiyo katika mabega yake mawili, moja akichora kichwa cha mnyama simba na jingine nembo ya klabu hiyo ya Msimbazi huku mkononi akiandika ‘Miss Simba Sport Club’.

Anasema tattoo zina gharama lakini hawezi kusema ametumia kiasi gani kwa kuwa ni zile zisizofutika.

“Siwezi kusema zimenigharimu shilingi ngapi maana ni pesa nyingi naweza kuwatisha wengine wenye mapenzi kama yangu, hizi tattoo ni za kudumu hazifutiki kabisa maisha yangu yote.”

ALITAMANI

KUcheza soka

“Napenda sana kucheza mpira, ila nimechelewa kutambua hilo pia mazingira niliyokuwa naishi hapo zamani, ya kijijini yalikuwa magumu kwa mtoto wa kike kucheza mpira wa kiume.”

HAWEZI KuSAHAU

Anasema mechi kadhaa hawezi kuzisahau ambazo zikiweka rekodi nzuri na mbaya kwa Simba, kwa kuwa hazitaondoka kwenye maisha yake ya ushabiki na imebakia kuwa historia.

Anasisitiza kuwa, hawezi kuisahau mechi ya Simba na Nkana iliyopigwa Disemba 2018 na Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam na kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Pia na mechi ya Simba vs As Vita ambayo tulishinda goli 2-1 siwezi kusahau kabisa.’’

UD SONGO VIPI?

Baada ya mafanikio ya msimu uliopia ambao Simba walifika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa, mashabiki walikwa na matumaini makubwa ya kufika mbali zaidi msimu huu.

Aggy alikuwa kati ya mashabiki waliokuwa na matumaini makubwa wakitembea vifua mbele.

Alipuuza gharama, alipuuza maumivu ya sindano za moto, akajitosa kuchora tattoo hizo za Simba na akaenda uwanjani kwa kujiamini kwamba Simba itafanya vizuri zaidi msimu huu.

Lakini UD Songo siyo watu wazuri. Wakaing’oa Simba katika hatua ya awali baada ya sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa, shukrani kwa bao la ugenini la ‘frii-kiki’ la winga Luis Miquissone aliyekuwa amevaa kitamba cha unahodha siku hiyo.

Tangu hapo, Simba ikamsajili winga huyo mwenye kipaji.

“Siwezi kusahau mechi ya Simba vs UD Songo. ndo mechi iliyoniumiza sana, Wanasimba tulikuwa na mategemeo makubwa ya kufika mbali, hadi nikachorarudi hizi tattoo, wao wakatuondoa katika ramani.”

CHANGAMOTO

SAFARINI

Aggy anasema anasafiri sana kwenda kuipa sapoti timu yake hiyo inapocheza nje ya Dar es Salaam.

Anasema wawapo safarini wanakuwa wengi na jinsia tofauti, kikubwa zaidi yeye anajitambua na kujua nini kinachomfanya asafiri na sio kitu kingine, hivyo anaheshimiana na kila mtu ndani ya safari.

“Changamoto kila sehemu zipo tu, ila ni za kibinadamu ambazo hata kutokusafiri utakabiliana nazo kwasababu mimi ni mwanamke, kikubwa ni kutambua uko pale kwaajili gani na kufuata kile kilichokupeleka na kuisapoti timu yetu pendwa.’’

KIKOSI CHAKE BORA SIMBA

Anasema, kikosi chake bora ni cha msimu uliopita 2018/19, chini ya Kocha Patrick Ausseums ambaye alionekana kuwafanya wachezaji wakaelewana na kuzoeana na kuwapa raha Wanasimba.

Anakitaja kikosi cha mauaji kilichomwangamiza Nkana kuwa ni Aishi Manula, Nicolas Gyan, Mohammed Hussein, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, James Kotei, Jonas Mkude Clatous Chama, Meddie Kagere, John Bocco pamoja na Emannuel Okwi

Wachezaji wa akiba katika mchezo huo walikuwa, Deogratius Munishi, Juuko Murshid, Said Ndemla, Shiza Kichuya, Rashid Juma na Hassan Dilunga.