Misosi hii inawapa nguvu wanasoka

Muktasari:

Mchezo wa soka unakukumbana kimwili pamoja na kusukumana kwa kupigana vipushi wakati wa kukabana au kunyang’anyana mipira uwanjani.

Mchezo wa soka ni moja ya michezo ambayo unahitaji kuwa na nguvu ili kuweza kumudu kucheza dakika zote 90 na huku pengine wanasoka wakihitajika kufanya hivyo kila wiki.

Jaribu kupata picha tu kwa wanasoka wanaoshiriki mashindano ya klabu bingwa UEFA katika michezo iliyochezwa wiki hii - wanasoka hao kesho na keshokutwa wana kibarua cha ligi.

Wachezaji hao nguvu hizo za kucheza mechi hizo zenye ushindani na huku wakirudi tena katika ligi zao za ndani wanazipata kwa kula lishe yenye wanga wakifuata mwongozo wa wataalamu lishe za michezo.

Wanasoka wanahitaji mlo unaowapa nguvu ili kuweza kukimbia kwa kasi, kuwa na utimamu kimwili na kudumu mchezoni kwa muda mrefu wakiwa imara.

Wakati wa kucheza mchezaji hupoteza nguvu nyingi, hivyo baada ya mchezo huhitaji mlo wenye nishati ili kurudisha nguvu iliyopotea ambayo huhifadhiwa mwilini.

Mchezo wa soka unakukumbana kimwili pamoja na kusukumana kwa kupigana vipushi wakati wa kukabana au kunyang’anyana mipira uwanjani.

Kuukimbiza mpira na kushambulia kwa kasi ni lazima nguvu itumike sana.

Siri kubwa ya kuweza kufanya hayo ni vyakula vya wanga ndivyo vinavyotupa nguvu na joto mwilini.

Wakati natazama michezo ya UEFA wiki hii niliona kukurukakara kadhaa za kutumia nguvu kiasi cha kusababisha kutolewa kwa mshambuliaji wa Chelseakutokana na majeraha alilopata Wakati wakikabana na beki wa klabu ya Valencia.

Haikuishia katika mchezo huo wa mapema wa UEFA, bali pia Liverpool walilazimika kumtoa mapema kiungo wao mwenye nguvu, Fabinho kutokana na kuangukiwa gotini na kiungo wa Napoli.

Matukio yote haya ni ya kawaida kabisa katika soka lenye ushindani ambalo siri kubwa ya guvu wanazotumia wanasoka hao ni mlo wa wanga.

Vyakula vya wanga kitaalamu hujulikana kama carbohydate - ni vyakula ambavyo vikiliwa pamoja na makundi mengine ya vyakula kwa uwiano uliozingatia kanuni za lishe huleta matokeo mazuri kwa mchezaji.

Vyakula vya wanga viko ndani ya makundi saba ya vyakula mengine ni pamoja na protini, mafuta, vitamini, vyakula vya nyuzinyuzi, madini na maji.

Aina ya vyakula vyenye wanga kwa wingi ni kama vile viazi, ugali, wali, mihogo, tambi, mikate, ndizi mbichi, maboga na viazi vikuu. Vyakula hivi vikivimeng’enywa hupatikana kiasi kikubwa cha sukari ukilinganisha na vingine.

Kwa kawaida vyakula tunavyokula huingia mwilini na kuchakatwa na kupata zao la sukari kitaalamu glucose - zao hili ndilo chanzo cha mwili cha kupata nishati inayowezesha mwili kufanya shughuli.

Sukari ndiyo kama mafuta au petroli inayotumiwa na mwili kuendesha mambo mbalimbali ukiwamo utendaji wa ubongo na shughuli za kimwili.

Sukari huweza kuhifadhiwa katika ini na misuli, na kutumika baadaye kama nishati ya akiba pale mwili unapohitaji kufanya shughuli mbalimbali ikiwamo kutembea, kukimbia, kuongea na kufikiri.

Ukiacha wanga, protini ya kwenye misuli na mafuta ya mwili ni chanzo cha kupata sukari (nishati). Kama utakula kiasi kidogo cha wanga mwili itabidi utumie vyanzo vya protini na mafuta kupata sukari.

Kama utakula wanga wa kutosheleza ina maana ile protini ya kwenye misuli haitatumiwa kama chanzo cha sukari, badala yake protini itabaki katika kazi yake ya kujenga na kukarabati mwili. Matokeo yake ni misuli kujijenga na kuwa imara.

Vyakula vya wanga vinamwezesha mwanasoka kuwa na uwezo mkubwa anapocheza kwani vyakula hivi hupunguza mchoko (fatigue), hivyo kumfanya adumu mchezoni kwa muda mrefu.

Wanamichezo huwa ni tofauti na mtu wa kawaida, wao wanatakiwa kula mlo kamili utakaompa nguvu na kumjenga mwili. Ulaji wake huwa ni wa ratiba, kupangiwa kiasi na aina ya chakula kwa kila mlo.

Hii inafanyika hivyo ili kumuepusha kupata uzito uliokithiri au kumnenepesha.

Uzito mkubwa au unene unaweza kumfanya mchezaji kushindwa kuhimili vishindo vya mchezo anaoshiriki, kushuka kiwango au kutopanda kiwango cha uchezaji.

Ili kuepukana na hali kama hizo mchezaji atahitaji kuepuka kula kiholela vyakula vya mtaani ikiwamo nyama choma, chips mayai na soda au vinywaji vya kutengenezwa viwandani.

Vyakula kama hivi vina wanga kiasi kikubwa, mafuta mengi na sukari nyingi na pia baadhi vinatayarishwa bila kufuata kanuni za afya.

Siyo tatizo kwa mchezaji kula chipsi zilizokaangwa na mafuta kiasi na yaliyothibitishwa kuwa ni salama, kwa kuwa chipsi zina kiasi kikubwa cha wanga na kupikwa na mafuta ni faida kwao kula kwa kiasi.

Ulaji wa sima yaani ugali mkubwa, ni vizuri mchezaji kula kuendana na mahitaji ya mwili na mazoezi anayofanya. Ndiyo maana tunashauri kuwepo na udhibiti wa uzito wa mwili wa mchezaji.

Kama unakula ugali mkubwa ambao ni wanga halafu unafanya mazoezi hafifu maana yake utakuwa na mlimbikizo wa sukari isiyotumika ambayo baadaye mwili huibadili na kuwa mafuta na kuhifadhiwa. Jambo hili ndilo linalozaa uzito uliokithiri au unene.

Ndiyo maana wataalamu wa tiba za michezo duniani hushauri klabu kuwa na wataalamu wa lishe za wanamichezo ambao ndio huwapa maelekeo ya ulaji sahihi wa vyakula ikiwamo wanga kwa usahihi kuendana na uhitaji wa mwili wa mchezaji.

Klabu za soka mbalimbali duniani ambazo zimepiga hatua kimaendeleo zimeajiri wataalamu hao - lengo ni kuhakikisha wanasimamia kitaalamu lishe za wachezaji wao.

Ieleweke kuwa pamoja na vyakula vya wanga kutupa nguvu na joto lakini endapo mazoezi ya mchezaji yasipokuwa na uwiano na mlo wa wanga anaokula huweza kumnenepesha na kumpa uzito mkubwa mwilini hivyo kumfanya kukosa wepesi wakiuchezaji.