Misimamo yamuondoa Drogba Caf

Muktasari:

Drogba ameichezea timu ya taifa ya Ivory Coast Jumla ya michezo 105 na ameifungia mabao 65 yanayomfanya awe mfungaji bora wa muda wote wa taifa hilo.

MSIMAMO wa nyota wa zamani wa timu ya Taifa ya Ivory Coast na Chelsea, Didier Drogba kutounga mkono uongozi wa Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf), Ahmad Ahmad umetajwa kuwa sababu kuu iliyopelekea staa huyo nguli wa soka kuenguliwa katika nafasi yake ndani ya shirikisho hilo.

Hivi karibuni kuliibuka taarifa kuwa Ahmad ameamua kumuweka kando Drogba aliyemteua kuwa mmoja wa washauri wake kutokana na mwanasoka huyo kushindwa kutimiza majukumu ya nafasi yake pia kutohudhuria wala kushiriki shughuli mbalimbali za shirikisho hilo.

Hata hivyo, mwandishi wa habari mkongwe, Mamadou Gaye aliyefichua uamuzi wa Ahamd kumuondoa Drogba kama mmoja wa washauri wake, amefichua kuwa uhusiano usioridhisha baina ya wawili hao umepelekea kwa kiasi kikubwa uamuzi huo.

"Kinachokoleza zaidi suala hilo la Drogba kuondolewa ni uungaji wake mkono kwa Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino ambaye amekuwa hafurahishwi na Ahmad," alisema Gaye.

Katika nafasi hiyo ya mshauri wa Rais Ahmad, Drogba jukumu lake kubwa ambalo alihitajika kulifanya ni kutafuta mawasiliano na wataalam sambamba na kufanya kazi kwa ukaribu na wanasoka wa zamani waliowahi kutamba barani Afrika ili kusaidia kuimarisha mchezo wa soka barani humu.

Uteuzi huo ulifanyika mwishoni mwa Julai mwaka jana mara baada ya kumalizika kwa Fainali za Mataifa ya Afrika zilizofanyika Misri.

Kabla ya kuteuliwa huko, Drogba alikuwa katika mipango ya kuwania nafasi ya Urais ndani ya Shirikisho la Soka Ivory Coast (FIF)