Mirambo: Uturuki kumetupa fundisho

Muktasari:

Serengeti Boys imepangwa Kundi A, pamoja na timu za Nigeria, Angola na Uganda huku kundi B, likiwa na Guinea, Cameroon, Morocco na Senegar.

KOCHA wa timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 'Serengeti Boys', Oscar Mirambo amesema mechi walizocheza Uturuki, michuano maalumu ya Uefa Assist zitawapa matokeo mazuri katika mashindano ya Afcon yatakayopigwa hapa nchini.
Serengeti Boys ambayo ilicheza mechi tatu, iliambulia ushindi wa mchezo mmoja tu walipoifunga Australia mabao 3-2, kisha ikapoteza kwa wenyeji Uturuki kwa mabao 5-0 na Guinea ilianza kuwachapa kwenye mechi ya ufunguzi kwa bao 1-0.
Oscar amesema mechi hizo zimewafaidisha kwa mambo mengi ikiwama kuwajua wapinzani wao kwenye Afcon.
"Ukiachana na wapinzani wetu ambao kwa sasa hawatakuwa wageni kwetu, vijana wamepata uzoefu wa kucheza mechi za kimataifa na kuzoea mazingira ya ushindani makubwa," alisema Oscar.
Serengeti Boys imepangwa Kundi A, pamoja na timu za Nigeria, Angola na Uganda huku kundi B, likiwa na Guinea, Cameroon, Morocco na Senegar.
Kikosi hicho kimerudi na kinaendelea na kambi yao jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mashindano hayo.