Miraji awatangazia vita makipa

Muktasari:

 Kabla ya kupata majeraha akiwa anaitumikia timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ katika mashindano ya Chalenji mwaka jana huko Uganda, Miraji Athuman alikuwa ameifungia Simba mabao sita katika mechi 10 alizoichezea.

Mshambuliaji wa Simba, Miraji Athuman ametoa tahadhari kwa makipa na mabeki wa timu za Ligi Kuu nchini kuwa ataendeleza makali ya kufumania nyavu pale ligi itakaporejea baada ya kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu.

Nyota huyo wa Simba, hajaonekana uwanjani tangu Disemba mwaka jana baada ya kupata majeraha ya kifundo yaliyomuweka nje kwa miezi mitano sasa ingawa siku za hivi karibuni ameanza mazoezi baada ya kupona moja kwa moja maumivu hayo.

Miraji aliyesajiliwa na Simba kabla ya msimu huu kuanza akitokea Lipuli, alisema kuwa pindi ligi itakaporejea, anaamini atakuwa sawa na makali yake yatarudi.

"Kwa muda mwingi nimekuwa nje ya uwanja kutokana na kuwa majeruhi, naendelea vizuri kwa sasa na nina imani ligi itakaporejea nitakuwa fiti zaidi. Kocha (Sven Vandenbroeck) amekuwa akinipa mazoezi binafsi ili niwe fiti zaidi" anasema Miraji.

Nyota huyo ni miongoni mwa kundi kubwa la wachezaji wa timu mbalimbali ambao siku za hivi karibuni wamekuwa wakifanya mazoezi katika ufukwe wa Coco Beach jijini.

Katika mazoezi yaliyofanyika leo, Miraji na nyota mwenzake wa Simba, Paschal Wawa ndio walikuwa wakiongoza mazoezi hayo kwa kuwaelekeza wenzao namna ya kufanya na kushiriki program kadhaa za kujiweka fiti ufukweni hapo.

Asilimia kubwa ya mazoezi waliyokuwa wakifanya ni kukimbia pamoja na kuruka kwa wachezaji hao ambao walikuwa zaidi ya 10.

 Kabla ya kupata majeruhi hayo, Miraji alikuwa ameifungia Simba mabao sita huku akipiga pasi mbili zilizozaa mabao.