Miquissone apewa jukumu zito Msumbiji

Muktasari:

Msumbiji iko kundi F la kuwania kufuzu Fainali za Afcon 2021 sambamba na timu za Taifa za Cameroon, Cape Verde na Rwanda, ikiongoza na pointi zake nne (4)


Nyota wa Simba, Luis Miquissone atakabiliwa na kibarua kigumu cha kuiongoza timu yake ya Taifa ya Msumbiji katika mechi mbili za kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) mwakani dhidi ya Cameroon zitakazochezwa kati ya Novemba 9 na Novemba 17 mwaka huu.

Miquissone ni miongoni mwa nyota 23 walioteuliwa na kocha wa timu ya taifa ya Msumbiji, Luis Goncalves kuunda kikosi hicho ambacho kitaanza kuikabili Cameroon 'Simba Wasioshindika' ugenini huko Yaounde, Novemba 9 na kisha kurudiana jijini Maputo, Msumbiji, Novemba 17.


Ushindi katika michezo hiyo miwili, utaihakikishia rasmi Msumbiji, tiketi ya kushiriki Afcon 2021 kwani itafikisha jumla ya pointi 10 ambazo zitaifanya isifikiwe na timu mbili kati ya nne zilizopo katika kundi lao G la mashindano hayo ya kufuzu.

Nyota wa Lille inayoshiriki LigI Kuu ya Ufaransa, Mandava Reinildoni miongoni mwa wachezaji wanaounda kikosi hicho cha Msumbiji ambacho pia kimemjumuisha mkongwe, Elias Domingues 'Pelembe' ambaye kwa sasa hana timu baada ya kuachana na Bidvest Wits ya Afrika Kusini ambayo kwa sasa imebadilishwa jina na inaitwa Tshakhuma FC.

Ni kikosi kinachoundwa na kundi kubwa la wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya Msumbiji huku wachache wakicheza ndani hasa wale wa safu ya ulinzi ambapo katika nafasi ya kipa, watatu walioitwa wanacheza katika ligi ya nyumbani.

Kundi kubwa la nyota waliopo nje ya nchi linahusisha wale wanaocheza soka la kulipwa nchini Ureno ingawa pia Ligi ya Afrika Kusini nayo imechangia idadi kubwa ya wachezaji.

Kikosi hicho cha nyota 23 wa Msumbiji kitakachoikabili  Cameroon kinaundwa na makipa José Guirrugo (UD Songo), Victor Guambe (Costa do Sol) na Júlio Frank (Ferroviário Maputo) wakati mabeki ni Bonera (CS Maritimo ) Zainadine Júnior (Maritimo), Sidique Sataca (UD Songo), Bheu (UD Songo) , Edmilson Dove (Cape Town City), Reinildo Mandava (Lille FC), Chico (TS Sporting FC) na Simao (Vegalta Sendal)

Viungo ni Nene (Costa do Sol), Telinho (UD Songo), Kito (Ferroviaro Maputo), Geny Catamo (Sporting CP), Kambala Manuel (Baroka FC), Elias Domingues na washambuliaji ni Amâncio Canhemba (Vitória de Setúbal), Witiness Quembo (Nacional), Clésio Bauque (FC Gabala), Stanley Ratifo (CfR Pforzheim), Luis Miquissone (Simba), Reginaldo Fait (FC Kaysar)