Minziro ageuka lulu Mbao

Muktasari:

Felix Minziro ameiongoza Mbao FC kupata ushindi katika mechi tatu za Ligi Kuu dhidi ya timu za Polisi Tanzania, Coastal Union na Lipuli ambazo zote imeibuka na ushindi

Winga wa Mbao FC, Herbert Lukindo ametamba kuwa iwapo kocha Felix Minziro angeanza mapema kuinoa timu hiyo, leo hii isingekuwa katika nafasi mbaya kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Mbao FC iko nafasi ya 19 katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 32 na iwapo itamaliza katika nafasi nne za mwisho itashuka daraja.

Akizungumza na Mwanaspoti,Lukindo alisema kocha huyo ameweza kuwabadilisha ndani ya muda mfupi kitu ambacho kimewafanya wawe bora sana tofauti na mwanzo.

“Niseme tu tumebadilika kwa sasa. Kiuchezaji Minziro kwa kipindi kifupi alichokuja ametupa ufundi mwingi sana. Ni bonge la kocha huyo na kama tungekuwa naye tangu mwanzo basi sasa tungekuwa moja ya timu bora sana Ligi Kuu.

Tutaendelea kusikiliza kwa umakini na kufuata mazoezi anayotupa ili kuweza kuwa fiti katika kipindi hiki tunapambana kuibakisha Ligi Kuu  hii timu msimu ujao kwani bado tuko katika nafasi mbaya kwenye msimamo,” alisema Lukindo.

Winga huyo alisema bado wana kazi nzito ya kuhakikisha wanapata ushindi katika mechi tano zilizosalia ambazo ndizo zitawaweka katika nafasi nzuri ya kutoshuka daraja msimu ujao.

“Tukishinda mechi tano zilizobaki basi hapo tutakuwa tumemaliza kazi maana tutakuwa tuko katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi kikubwa tutaendelea kupambana,” alisema Winga huyo.