Minziro, Waziri Jr wabeba tuzo

Muktasari:

Baada ya kufanya vizuri msimu huu, uongozi wa klabu ya Yanga uliamua kumsajili mchezaji huyo kwa kumpa mkataba wa miaka miwili.

ALIYEKUWA mshambuliaji wa Mbao FC, Waziri Junior amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Julai wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2019/20 huku kocha Fred Felix Minziro wa timu hiyo akichaguliwa kuwa Kocha Bora wa mwezi huo.

Junior msimu huu akiwa na timu hiyo amekuwa bora baada ya kufunga magoli 13 mpaka Ligi inamalizika na magoli mawili katika Play-off dhidi ya Ihefu.

Hii inakuwa ni tuzo ya pili kwa msimu huu kwani awali alichukua tuzo ya mchezaji bora mwezi Novemba.

Waziri na Minziro wametwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzao walioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki hii na Kamati ya Tuzo za VPL zinazotolewa na TFF.

Kwa mwezi huo wa Julai, Mbao ilicheza michezo sita, ikashinda mitano na kupata sare moja, huku Waziri Junior akiwa sehemu kubwa ya mafanikio hayo, akifunga mabao matano na kutoa pasi moja ya mwisho.

Waziri amewashinda Peter Mapunda wa Mbeya City na Obrey Chirwa wa Azam FC alioingia nao fainali.

Mapunda aliisadia timu yake kushinda michezo minne kati ya sita waliyocheza mwezi huo, akifunga mabao matatu na kutoa pasi mbili za mwisho, wakati Chirwa alifunga mabao manne yalioisaidia Azam kushinda michezo mitatu na kupata sare mbili katika michezo sita.

Kwa upande wa Minziro, amewashinda Amri Said wa Mbeya City na Aristica Cioaba wa Azam, ambapo Minziro aliiongoza Mbao kushinda michezo mitano kati ya sita waliyocheza ndani ya mwezi Julai na kupata sare moja.

Amri Saidi kwa upande wake aliiongoza Mbeya City kushinda michezo minne kati ya sita, huku Cioaba akiingoza Azam FC kushinda michezo mitatu, sare mbili na kupoteza mmoja.