Milioni 5 za Mengi zabebwa dakika 22 tu!

Monday April 15 2019

 

By Thobias Sebastian

ACHANA na matokeo ya kuanza vibaya kwenye mchezo wao wa kwanza wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) U17, vijana wa Serengeti Boys wameibeba Sh 5 milioni za Mlezi wao, Reginald Mengi aliyeahidi kuitoa kwa mchezaji atakayefunga bao la kwanza la timu hiyo.

Edmund John ndiye aliyevuna fedha hizo baada ya kufunga bao la kusawazisha dakika ya 22 tu ya mchezo huo ambao Nigeria waliibuka na ushindi wa mabao 5-4 na hivyo kujihakikishia kubeba mkwanja huo alioahidi Mengi ambaye pia ameahidi gari kwa kila kama watafuzu Fainali za Dunia U17.

Katika mchezo huo uliokuwa mkali, Nigeria walionekana kuizidi Serengeti katika kipindi cha kwanza ambacho kilishuhudia Nigeria wakiongoza kwa mabao 3-1.

Nigeria ndio walikuwa wa kwanza kulisalimu lango la Serengeti kwa shambulizi la Ayobami aliwekewa pasi ya mwisho na kukutana na kipa wa Serengeti Boys, Mwinyi akaupangua mpira huo ndipo dakika ya 21 Olatomi Olaniyan ambaye alikutana na mpira uliopigwa shuti kali na kupanguliwa na kipa.

Dakika moja baadaye Serengeti ilirejesha bao hilo kupitia kwa Edmund kabla ya mabingwa hao mara mbili wa michuano hiyo kufunga mabao mengine mawili kupitia kwa Wisdom Ubani dakika ya 30 na Akinkunmi Amoo dakika ya 37.

Kipindi cha pili Serengeti ilirejea kwa kasi na kurejesha mabao hayo kwani dakika ya 52 Kelvin Pius alipiga shuti kali lilimshinda nguvu kipa wa Nigeria kabla ya Edmund na nahodha Abraham Maurice kufunga mkwaju wa penalti dakika ya 58 kuisawazishia Tanzania.

Dakika mbili baadaye Edmund alifunga penalti kifundi baada ya beki wa Nigeria kuunawa mpira langoni mwake na kuifanya Serengeti kuwa mbele kwa mabao 4-3 na kuwafanya mashabiki kuliamsha shangwe mwanzo mwisho kwa kuamini timu yao inatoka na ushindi.

Hata hivyo, makosa yale yale ya mabeki wa Serengeti yaliifanya timu hiyo kujikuta ikifungwa mabao mawili ndani ya dakika chache na kuwapa ushindi Nigeria ambao nyota wake, Ubani aliyefunga dakika 72 na Ibraheem Jabaar kumaliza udhia dakika ya 78.

Kocha wa Serengeti, Oscar Mirambo amesema licha ya kupoteza wanaenda kujipanga kwa mchezo wao ujao dhidi ya Uganda na ana imani watasahihisha makosa kwani amebaini kikosi chake kilikuwa na upungufu anayoenda kuufanyia kazi kuhakikisha mechi zao zilizosalia wanashinda na kuvuka.

“Matokeo hayo yametuchanganya, lakini ndivyo soka lilivyo, tunaenda kujipanga kwa mchezo wetu ujao dhidi ya Uganda kabla ya kumalizana na Angola, tunaamini tutavuka kutinga nusu fainali, bado tuna nafasi,’ alisema Mirambo.

Advertisement