Mikono ya De Gea yampagawisha Solskjaer

Muktasari:

  • Ole Gunnar Solskjaer amekuwa kocha wa kwanza wa Man United kushinda mechi sita za mwanzo za kibarua chake baada ya Marcus Rashford kufunga bao pekee

London, England. Kocha wa muda wa Ole Gunnar Solskjaer amesema kipa David de Gea amethibisha mwenyewe kuwa ni moja ya makipa bora waliowahi kutokea Manchester United.

Kipa huyo Mhispania aliokoa hatari 11 na kuisaidia Man United kushinda 1-0 dhidi ya Tottenham kwenye Uwanja wa Wembley.

Katika miaka yake 11, aliyokuwa mshambuliaji ndani ya Old Trafford, Solskjaer alicheza pamoja na makipa bora Edwin van der Sar na Peter Schmeichel.

"Tumekuwa na rekodi ya kuwa na makipa bora katika klabu hii nafikiri anaweza kulinganana na Edwin na Peter katika orodha ya makipa bora katika historia ya klabu hii," alisema Solskjaer.

De Gea aliokoa mashuti 11 yaliyokuwa yanaelekea golini ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuwahi kutokea katika Ligi Kuu England huku akiendelea kulinda rekodi ya kutoruhusu wavu wake usiguswe na kuiongoza Man United kushinda mechi sita kati ya sita waliozkuwa chini ya Solskjaer.

Mhispania huyo alijiunga na Man United akitokea Atletico Madrid mwaka 2011 tangu wakati huo amefanikiwa kushinda tuzo ya mchezaji bora wa klabu hiyo mara nne katika misimu mitano iliyopita.

"Tuna mabeki wanne wazuri na David yupo nyuma yao ni kitu usichokitegemea. Tumekuwa na bahati ya kuwa na kipa bora.

Ushindi huo wa tano mfululizo wa Ligi Kuu chini ya Solskjaer inafanya Man United inayoshika nafasi ya sita kuwa sawa kwa pointi na Arsenal inayoshika nafasi ya tano, huku wakiwa nyuma kwa pointi sita kuingia katika nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa.