Migne bado yuko area mbaya joh

Muktasari:

Shirikisho la soka nchini FKF liliamua kumchuja kazi Migne kutokana na uzalishaji wa matokeo dunia hasa baada ya kubanduliwa nje ya dimba la CHAN 2020 na Tanzania, timu ambayo wadau wengi wa soka nchini waliitaja kuwa hafifu mno.

BAADA ya kuchujwa wera kama Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa Harambee Stars, wiki mbili zilizopita, ungelitegemea kuwa sasa hivi Kocha Mfaransa, Sebastian Migne angelikuwa tayari alishatua nyumbani kwao Ufaransa.

Hata hivyo, kocha huyo bado yupo mjini Nairobi na anasema wala hana haraka ya kuondoka licha ya kuwa hana kazi ya kufanya kwa sasa. Migne kasisitiza kuwa bado yupo area ile mbaya kisa familia yake.

“Mimi bado nipo huku wala sijawa wa kuondoka. Familia yangu imelipenda Jiji la Nairobi hivyo tutakuwepo kwa muda,” kasema Migne.

Shirikisho la soka nchini FKF liliamua kumchuja kazi Migne kutokana na uzalishaji wa matokeo dunia hasa baada ya kubanduliwa nje ya dimba la CHAN 2020 na Tanzania, timu ambayo wadau wengi wa soka nchini waliitaja kuwa hafifu mno. Kutemwa huko wadau hao waliohoji kuwa Migne kaonyesha waziwazi kwamba hawezani na kazi.

Wadau hao ambao ndio waliosababisha yeye kutimiuliwa walihoji kuwa hapakuwepo na sababu zaidi za kuendelea kumlipa Migne pamoja na wasaidizi wake wawili mamilioni ya pesa wakati ipo wazi kwamba kazi imemlemea.

Migne alikuwa akilipokea mshahara wa Sh1.5 milioni kila mwezi na mkataba wake na Stars ulikuwa ungali una miaka miwili zaidi. Wasaidizi wake wawili wa Kizungu nao walikuwa wakipokea nusu milioni kila mmoja wao kama mishahara.

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita FKF tayari wameshapoteza kesi mbili baada ya kuwavunjia mikataba makocha wawili kabla ya muda.

Mahakama ya Kimichezo yenye makao yake kule Lausanne, Swirtzerland CAS, iliiamrisha FKF kumlipa marehemu Kocha Mfaransa Henri Michel Sh4.5 milioni na Kocha Mbelgiji Adel Amrouche Sh60 milioni wote ambao mikataba yao ilikiukwa.