Migne anyoa wanne, akitangaza nyota 23 Afcon Misri

Tuesday June 11 2019

 

By Fadhili Athumani

Nairobi. Hatimaye kitendawili cha nani watapeperusha bendera ya Kenya, katika makala ya 32 ya Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON 2019, zitakazofanyika huko Misri, kimeteguliwa mapema leo baada ya mazoezi ya Harambee Stars, iliyoko kambini Jijini Paris, Ufaransa.

Baada ya majumaa mawili ya kukitizama kikosi cha wachezaji 27 kilichokuwa kambini, Kocha mkuu wa Harambee Stars, Mfaransa ameridhika kuwa Clifton Miheso na Anthony 'Teddy' Akumu, hawatoshi mboga.

Nyota wengine waliopitiwa na panga la Mfaransa huyo, kiungo mshambuliaji Christopher Mbamba na beki wa kati Brian Mandela, ambao ni majeruhi. Mbamba amekuwa majeruhi tangu siku ya kwanza ya kambi, juhudi za kutibu jeraha lake la enka, zimegonga mwamba.

Mandela aliyekuwa ni beki tajika katika kikosi cha Migne, aliumia jana wakati wa mazoezi ya asubuhi. Katika nafasi yake, Migne hana budi zaidi ya kumtegemea beki wa Gor Mahia Joash Onyango, ambaye msimu huu amekuwa katika kiwango cha juu.

Ikumbukwe kwamba, Chris Mbamba, mwenye umri wa miaka 27, mzaliwa wa Zimbabwe, Babake akiwa ni Mnamibia na Mama Mkenya, alikuwa na matumaini ya kuvaa jezi la Kenya kwa mara ya kwanza baada ya kuwatolea nje Sweden.

Hata hivyo, habari nzuri ni kwamba, beki wa kati Musa Mohamed na Winga Ayub Timbe, walioumia kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Madagascar, wanaendelea vizuri na wamejumuishwa kwenye kikosi kinachoenda Misri, lakini watakosa mchezo wa kirafiki dhidi ya DR Congo.

Advertisement

Kwa maana hiyo, Kenya itawakilishwa na nyota 23, ambao Juni 15, wataivaa DR Congo katika mchezo wa pili wa kujipima nguvu. Mechi hii itapigwa nchini Hispania, katika Jiji la Paris. Baada ya hapo, Juni 19 kikosi kitaelekea Cairo, Misri kwa ajili ya AFCON.

Kenya, inayoshiriki fainali hizi kwa mara ya kwanza baada ya miaka 15, iko katika kundi C, pamoja na Algeria, Senegal na majirani zao Tanzania, itatupa karata yake ya kwanza, Juni 23 dhidi ya Algeria, kisha itaivaa Taifa Stars (Juni 27), kabla ya kuumana na Simba wa milima ya Teranga, Julai mosi.

KIKOSI CHA MWISHO CHA STARS

Makipa: Patrick Matasi, John Oyemba, Faruk Shikalo

Mabeki: Philemon Otieno, Abud Omar, Bernard Ochieng, Musa Mohammed, Joash Onyango, Joseph Okumu, David Owino, Eric Ouma

Viungo: Victor Wanyama, Dennis Odhiambo, Erick Johanna, Ayub Timbe, Francis Kahata, Ismael Gonzalez, Ovella Ochieng, Paul Were, Johanna Omollo

Mastraika: Masud Juma, Michael Olunga, John Avire

Advertisement