Migne achimba mkwara, Ethiopia lazima wafe

Muktasari:

Harambe Stars inakutana na Ethiopia kesho ikiwa na matumaini makubwa ya kupata ushindi kama walivyofanya dhidi ya Ghana, miezi miwili iliyopita na kujiweka sawa katika Kundi F. Kwa sasa kikosi cha Sebastien Migne kinashika nafasi ya pili nyuma ya Ghana.

Nairobi, Kenya. Kocha wa Harambe Stars, Sebastien Migne amewataka wachezaji wake kutofanya makosa kabisa kuhakikisha washinda mechi ya kesho dhidi ya Ethiopia na kujiweka vizuri katika Kundi F katika kusaka tiketi ya kucheza fainali za mataifa ya Afrika, yatakayofanyika mwakani nchini Cameroon.

Harambee Stars itawavaa Ethiopia katika mchezo mkali, utakaopigwa ugani Badir Dar, nchini Ethiopia, ambapo vijana wanahitaji ushindi kujiweka sawa katika kampeni za kusaka tiketi ya kwenda Cameroon.

Katika kuonyesha msisitizo, Migne amekuwa na rekodi nzuri, tangu achukue mikoba ya kuinoa Stars alisema amewataka wachezaji wake wafanye kile walichowafanyia Ghana, Jijini Nairobi na kuondoka na ushindi wa bao 1-0.

Kiburi cha Migne, kuelekea mtanange huo, unatokana na uwepo wa maproo wake wote 13, akiwemo Nahodha Victor Wanyama aliyekosa mechi ya Ghana, pamoja na Straika matata, Michael Olunga anayekipiga nchini Japan.

 “Mchezo dhidi ya Ghana, ulitupatia matumaini makubwa ya kwenda Cameroon, lakini kazi haijaisha bado, tunahitaji kushinda mechi ya kesho. Ethiopia nawajua sana, wana wachezaji wazuri, wana kasi na ari kubwa. Lakini kama tulifanikiwa kuwapiga Ghana, mbona tunaweza tu,” alisema Migne

Kikosi cha Harambee Stars:

Patrick Matasi (Tusker), Farouk Shikhalo (Bandari), Abdallah Hassan (Bandari), Philemon Otieno (Gor Mahia), Francis Kahata (Gor Mahia), Allan Wanga, (Kakamega Homeboyz), Piston Mutamba (Sofapaka), Patrick Matasi, Dennis Odhiambo (Sofapaka, Kenya), Benard Ochieng (Vihiga United).

Wengine ni Musa Mohammed (Nkana FC, Zambia), Brian Mandela (Maritzburg FC, South Africa), Abud Omar (Cercle Brugge, Belgium), na David Ochieng (IF Brommapojkarna, Sweden), Erick Ouma (Vasalund, Sweden), Ismael Gonzales (Las Palmas, Spain).

Nahodha Victor Wanyama (Tottenham Hotspurs, England), Anthony Akumu (Zesco United, Zambia), Johanna Omollo (Cercle Brugge, Belgium), Paul Were (FC Kaisar, Kazakhstan), Michael Olunga (Kashiwa Reysol), Erick Johanna (IF Brommapojkarna), Ovella Ochieng (Vasalund).